Mashaka Mgeta, Mtwara
Zaidi ya nusu ya eneo la misitu 12 inayosimamiwa na Serikali Kuu kupitia Wakala
wa Huduma za Misitu (TFS) mkoani Mtwara, ipo kwenye vyanzo vya maji,
ikiathiriwa na ukataji miti hovyo unaovifanya (vyanzo hivyo) kuwa katika hatari ya
kutoweka.
Idadi hiyo ni sehemu ya misitu 51 inayosimamiwa na TFS katika Kanda ya Kusini
yenye mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara. Kwa ujumla, ukanda huo wa kusini
mwa nchi una jumla ya hekta 1,492,000 za misitu, 11,600 kati ya hizo zipo mkoani
Mtwara.
Wakati Mtwara ikiwa na eneo hilo la misitu, Mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa
kuwa na hekta 744,000 ukifuatiwa na Lindi yenye hekta 581,000. Misitu hiyo ni ile
inayosimamiwa na TFS. Kwa uwiano huo, Mtwara ni mkoa wenye eneo dogo la
misitu ikilinganishwa na mikoa mingine katika ukanda wa kusini.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa, eneo kubwa la misitu ya Mtwara
linatumika kwa uhifadhi wa vyanzo vya maji, hivyo kuwa sababu ya wawekezaji
kutowekeza katika sekta ya viwanda vya mazao ya misitu hususani mbao mkoani
humo.
Kaimu Meneja wa TFS wa Kanda ya Kusini, Ebrantino Mgiye, amethibitisha
sehemu kubwa ya misitu hiyo mkoani Mtwara kutumika kwa uhifadhi wa vyanzo
vya maji, ikilinganishwa na ile inayofaa kwa uvunaji.
Mgiye amesema wakati Mtwara ikiwa na kiasi kidogo cha hekta za misitu katika
ukanda huo, eneo kubwa lenye hekta 64,857 lina misitu yenye kuhifadhi vyanzo
vya maji wakati hekta 50,776 ikifaa kwa uvunaji, hivyo kutokidhi mahitaji.
Amesema katika mazingira hayo, si rahisi kutegemea kuwapata wawekezaji katika
sekta ya viwanda vya mbao mkoani humo, kwa vile miti mingi inalindwa kwa
uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Mwekezaji mmoja katika viwanda vya mbao ambaye hakutaka jina lake
kuandikwa gazetini, amesema ni vigumu kuwekeza katika sekta hiyo mkoani
Mtwara kwa vile hakuna uhakika wa uzalishaji, sababu ikiwa ni kutokuwapo
upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo.
Wakati hali ikiwa hivyo, vitendo vya ukataji miti hovyo vimebainika kuendelea
kwenye misitu inayosimamiwa na TFS. Msitu mingine iliyopo mkoani humo ni ile
inayomilikiwa na halmashauri za wilaya na jamii za vijijini.
Uchunguzi wa JAMHURI umebainika kuwapo kwa sababu kadhaa zinazochochea
ukataji miti hovyo kwenye misitu ya TFS, ikiwamo umbali uliopo kati misitu na
mahali zilipo ofisi za Wakala huo.
Misitu mingi ya mkoani humo inayomilikiwa na TFS, inakadiriwa kuwa umbali wa
zaidi ya kilomita 45 kutoka zilizopo ofisi za Wakala huo.
Sababu nyingine ni ushiriki mdogo wa wananchi wanaoishi kwenye maeneo
yanayozunguka misitu hiyo kudhibiti vitendo vya ukataji miti hovyo, wengine
wakishirikiana na wavunaji haramu.
Mkazi wa wilayani Nanyumbu, Paschal Enzerone, amesema wananchi wanaoishi
kwenye maeneo ya kuzunguka misitu, wasiposhirikishwa katika ulinzi ushirikishi,
inakuwa vigumu kuwadhibiti wahusika katika hujuma hiyo.
Kwa mujibu wa Enzerone, ushiriki wa jamii hizo unapaswa kufanyika kwa mfumo
unaozinufaisha pande zote, ili kuongeza ari na motisha katika udhibiti dhidi ya
ukataji miti hovyo.
“Wananchi wanaoishi maeneo ya kuzunguka misitu ni muhimu sana kufanya ulinzi
dhidi ya wanaoihujumu rasilimali hiyo, wakiachwa pembeni ama kutonufaika
kutokana na ushiriki wao.
Kutumika kama kiwanda
Kaimu Meneja wa TFS, Mgiye, amesema licha ya sehemu kubwa ya misitu
kutumika kwa uhifadhi wa maji, bado inaweza kutunzwa, kulindwa na kuwa kivutio
cha utalii.
Mgiye amesema misitu michache inayoruhusiwa kwa uvunaji, inaboreshwa zaidi
na kuwa soko la ajira kwa watu watakaofanya kazi za kuitunza, kupanda miche
mipya na kushiriki uvunaji halali.
“Unapoanzisha shamba la miti linakuwa sawa na kiwanda kwa maana
linatengeneza ajira kwa shughuli za kuanzia utayarishaji, upandaji miti, kuhudumia
na uvunaji wa mazao yake,” amesema.
RC: Kuna uhaba wa rasilimali za misitu
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, amesema miongoni mwa mambo
ya msingi katika kuifanya sekta ya misitu kuchangia Tanzania ya viwanda, ni wingi
na upatikanaji endelevu wa rasilimali za misitu hususani mbao.
Amesema kwa hali ilivyo sasa, upatikanaji wa mbao katika mkoa wa Mtwara upo
kwa kiwango kisichotosha kutegemewa kwa uanzishwaji wa viwanda vya mbao
ama mazao mengine ya misitu.
Byanakwa amesema ipo haja kwa Serikali kufanya tathmini ya kina kubaini
ukubwa wa misitu, idadi ya miti na aina zake ili uzalishaji wake uwezeshe
upatikanaji endelevu wa bidha za viwandani na uhitaji wake kwa soko la nje ya
nchi.
Kuhusu hatari ya kutoweka kwa miti, Byanakwa amesema ipo haja kwa
wafanyabiashara wanaohusika na ukataji miti kwa shughuli za kibiashara kama
utengenezaji mkaa, kupanda miti iliyo mahususi kwa ajili shughuli zao, vinginevyo
itakuwa vigumu kuzungumzia uwapo wa misitu endelevu.
“Ikiwa watu wataanzisha mashamba ya miti kwa ajili ya shughuli kama
utengenezaji wa mkaa, ni dhahiri kwamba kutakuwa na utaratibu halali usioharibu
misitu ya asili,” amesema.
Miti ya vipaumbele
Byanakwa amesema upandaji miti unaoratibiwa na TFS, unapaswa kuainisha aina
mahususi ya miti, kwa vile ipo mingine inayochukua muda mrefu tangu kupandwa
hadi kuvunwa.
Kama ilivyo kwa Mgiye, Mkuu wa Mkoa huyo amesema si sahihi kuwa kila msitu
unapaswa kuvunwa na mazao yake kutumika katika uendeshaji wa sekta ya
viwanda nchini.
“Misitu mingine kama ilivyo ya huku upande wa kusini hasa Mtwara, inaweza
kubaki kwa ajili ya utalii kwa vile sehemu kubwa ni hifadhi ya maji, makazi ya
wanyamapori na ndege vinavyoweza kuwa vivutio kwa utalii,” amesema.
Byanakwa amesema uzuiaji wa vitendo vya kukata miti hovyo havihitaji uelimishaji
umma, bali kuwapo mtazamo wa jamii kuhusu faida za rasilimali hizo na hasara
yake pindi zinapohujumiwa.
“Tukifika mahali kila mtu kabla hajakata mti kwa mahitaji yake, akajiuliza hivi
kesho akiuhitaji tena mti huo ataupata wapi, tukiwa na fikra hiyo basi kila mmoja
atashiriki kupanda miti kabla ya kukata,” amesema.
TFS yaongeza mashamba
Kwa upande wake, Mgiye amesema ili kukabiliana na hatari ya kutoweka kwa
misitu, TFS imeongeza mashamba mapya ya miti tangu kuanzishwa kwake 2011.
Kwa mujibu wa Mgiye, miongoni mwa mashamba mapya ya miti ni pamoja na
hekta 3,800 za msitu wa Wino Ifinga uliopo Madaba mkoani Ruvuma. Pia
wameongoza hekta 1,500 kutoka 7,000 zilizokuwapo kufikia 8,500 kwenye hifadhi
ya msitu wa Rondo.
Pia Mgiye amesema katika kipindi cha kuanzia Januari mwaka huu, TFS
imepanda miti kwenye hifadhi ya msitu wa Mpepo wenye ukubwa wa hekta 200.
Kiwango cha uvunaji
Mgiye anasema Tanzania ina uhitaji wa mita za ujazo milioni 62.3 za uvunaji
endelevu wa miti katika kipindi cha mwaka, lakini uwezo wa misitu uliopo ni kufikia
mita za ujazo milioni 42.8, hivyo kusababisha nakisi ya mita za ujazo milioni 19.5
Takwimu hizo zinatafsiri kuwa upungufu huo unazibwa kupitia ukataji miti hovyo
kwa misitu ikiwamo ya mkoani Mtwara.
Ni kutokana na hali hiyo, Mgiye amesema uwezo wa misitu ya asili kurejea katika
hali yake ya awali ni mdogo, akitolea mfano wa mti wa mpingo unaochukua
takribani miaka 100 tangu kupandwa hadi kuvunwa.
Anasema ili kuepuka kadhia hiyo, jamii inapaswa kuwekeza katika upandaji miti
inayochukua kati ya miaka 20 hadi 23 kuvunwa, akitolea mfano wa nchini Finland,
namna Taifa hilo lilivyowekeza katika sekta hiyo ndogo ya misitu.
Uharibifu wa kibinadamu
Mgiye amethibitisha kuwapo uharibifu wa misitu kwa njia za ukataji haramu wa
miti, hali inayoilazimu TFS kutumia doria za mara kwa mara kuwadhibiti
wanaojihusisha na uharibifu huo.
Kwa mujibu wa Mgiye, kuna hatua kadhaa za uvunaji kwa njia halali, ikiwamo
kutuma maombi kwa kamati za uvunaji zinazoongozwa na Mkuu wa Wilaya
(Mwenyekiti).
Hatua hiyo inafanyika baada ya mvunaji kukutana na wananchi wa kijiji kilichopo
karibu ama kuzunguka msitu anaohitaji kuvuna. Wananchi hao wana mamlaka ya
kumthibitisha ama kumkataa, kwa mujibu wa sheria ndogondogo walizojiwekea.
Wajumbe wanaounda kamati ya uvunaji katika ngazi ya wilaya ni Meneja Misitu
wa Wilaya wa TFS (Katibu), Afisa Misitu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya na
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili.
Wengine ni Afisa Misitu wa Wilaya, Afisa Mtendaji wa Kijiji (kinachopakana na
msitu utakaovunwa) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji (kinachopakana na
msitu utakaovunwa).
Tofauti na ukataji miti hovyo unapofanyika, uvunaji halali unawawezesha
kupatikana kwa tozo mbalimbali kulinganana daraja la miti, ambapo mvunaji
anathibitisha uhalali wake kupitia leseni anayokabidhiwa kwa ajili ya biashara
hiyo.
Mvunaji halali akikamilisha hatua hizo, anapaswa kuwa na nyaraka kadhaa wakati
akisafirisha mbao, miongoni mwa hizo ni leseni ya biashara, nyundo ya kuainisha
uhalali wa mbao, hati ya kusafirishia na hati za malipo.
Licha ya hali hiyo kufanyika kwa umakini, zipo taarifa zinazothibitishwa na Mgiye,
kuwapo watu wanaoghushi nyaraka kwa lengo la kuficha ukweli hasa
wanapojihusisha na ukataji miti hovyo.
Pia anasema wapo wavamizi wa maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo, akitolea
mfano hifadhi ya msitu wa Mbangala uliopo wilayani Nanyumbu.
“Misitu ina vizazi vyake ambavyo ni miti michanga, sasa inapoliwa na mifugo hasa
katika misitu iliyopo kwenye wilaya za Kilwa na Tunduru inakuwa tatizo kwa jamii,”
amesema.
Kiasi cha misitu kilichoharibiwa
Mgiye amesema utafiti pekee wenye kubaini kiasi cha uharibifu wa miti uliofanyika
katika misitu iliyopo mkoani Mtwara, ulifanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine na
kwamba matokeo rasmi bado hayajatolewa.
Ingawa ni hivyo, anasema inakadiriwa kuwa kiasi cha kati ya asilimia 20 hadi 30
ya misitu katika msitu wa Masasi Hills pekee, imeshaharibiwa kutokana na uvunaji
haramu.
Mbali na msitu huo, kielelezo kingine cha uharibifu wa misitu ni hatari ya kutoweka
kwa msitu wa Msanjesi ambao sehemu yake inasimamiwa na kijiji cha
Namalembo.
Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini Serikali katika wilaya ya Masasi
ilibaini hatari ya kutoweka kwa msitu huo na hivyo kuchukua hatua ya kuzuia
uvunaji miti.
JAMHURI liliwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee,
anayethibitisha kusimamishwa kwa ukataji miti wa aina yoyote kwenye msitu huo.
Mzee amesema moja ya wajibu wake ni kuzielekeza mamlaka husika, kuweka
mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwamo katika sekta ya misitu kwa kuyaelekea
maeneo kama mpango wa matumizi bora ya ardhi na ulipaji fidia kwa mujibu wa
sheria.
Amesema ingawa hali ya uhifadhi wa misitu kwenye sehemu kubwa ya wilaya
hiyo ni nzuri, baadhi ya maeneo yameharibika ikiwamo msitu huo
Kwa mujibu wa Mzee, usitishwaji mpango wa kukata miti kwenye msitu huo
umechukuliwa kutokana na kasi ya ukataji uliofanyika na kwamba utaendelea
ikiwa upandaji miti utafanyika kwa kiwango cha kuridhisha.
Mzee amesema ingawa azma ya Serikali ni kujiekeza katika uchumi wa viwanda,
lakini wilaya hiyo haiwezi kutumia kigezo hicho (uchumi wa viwanda) kuwekeza
katika ukataji miti usiokuwa na tija kwa jamii na mazingira.
Hata hivyo, Mzee anatahadharisha kuwa kumbukumbu za awali kuhusu ukataji
miti hovyo, hazipaswi kuwekwa wazi kwa vile zinaweza kuwakumbusha wahalifu
wa zamani na kuwaibua wengine wapya katika sekta hiyo.
Ernest Berdon, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, amesema ingawa hakuwapo wakati
wa utekelezaji wa agizo hilo, taarifa zinaonesha kuwapo kiwango kikubwa cha
ukataji miti hovyo, hali iliyohatarisha kuvurugika kwa amani na umoja kijijini hapo.
Taarifa zaidi zinazothibitishwa na Afisa Mtendaji huyo zinadai kuwa uharibifu wa
msitu huo hasa katika ukataji miti hovyo ulichangia kujiuzulu kwa uongozi wa kijiji
hicho uliokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Juma Ndembo.
Pia iliyokuwa kamati ya ardhi na maliasili ya kijiji hicho ilivunjwa, kutokana na
baadhi ya wajumbe wake kudaiwa kuwa washirika wa watu waliohusika katika
uharibifu wa msitu huo.
Michael Chitanda, aliyewahi kuwa Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji hicho, amesema
awali shughuli za usimamizi wa msitu huo zilifanikiwa kutokana na ushiriki mpana
wa jamii wakiwamo vijana.
Amesema ari ya usimamizi ilianza ‘kupotea’ kutokana na kuwapo taarifa
zilizowahusisha baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kushiriki katika uharibifu wa
misitu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo kilichopo kijijini hapo, Damian Joseph,
amesema msitu huo ulikinufaisha kijiji hicho hasa kwa mapato yaliyotokana na
tozo za mazao ya msituni, akitoa mfano wa mbao moja kutozwa ushuru wa
shilingi 1,000.
Amesema kwa kawaida, mfanyabiashara mmoja aliweza kuvuna na kulipa tozo ya
mbao zilizofikia 300 kwa safari moja. Joseph anasema lakini mwenendo wa
usimamizi wa msitu huo ulibadilika kutokana na uharibifu mkubwa uliofanyika.
Ingawa hakuna takwimu za utafiti wa ki-sayansi kwa kiwango cha uharibifu
uliofanyika, Joseph amesema inakadiriwa zaidi ya nusu ya msitu huo umeathirika
kwa ukataji miti hovyo.
“Siwezi kujua ni kiasi gani halisi cha msitu kimeathirika lakini tunapoingia
kuutembelea tunaona miti imekatwa hovyo kwa eneo la zaidi ya nusu hivi,”
amesema.
BIASHARA YA MBAO KWENDA MSUMBIJI
Moja ya changamoto zilizobainika na kuwa chanzo cha uharibifu wa misitu ya
mkoani Mtwara ni biashara haramu ya mbao zinazotokana na ukataji miti hovyo
kwenye misitu ya mkoani humo.
Mbao hizo zimebainika kusafirishwa kwa ‘njia za panya’ na kuingia ndani ya ardhi
ya Msumbiji, ukanda wa kaskazini mwa nchi hiyo, kisha kurejeshwa nchini, lengo
likiwa ni kuficha ukweli kuhusu ukataji miti haramu ulivyofanyika.
Eneo la kaskazini mwa Msumbiji linaelezwa kuwa na misitu. Inakadiriwa kuwa
umbali wa kutoka mpaka wa Mtambasalwa hadi wilaya ya Mueda katika mkoa wa
Cabo Delgado nchini Msumbiji ni takribani kilomita 240.
JAMHURI limebaini kuwa tawala za mikoa nchini Msumbiji, ziliwasilisha ombi la
matumizi ya baadhi ya mipaka zaidi ya ule wa Mtambasalwa, ili kuwezesha
upitishaji mizigo kwa urahisi kwa vile barabara inayotoka mpakani hapo kuingia
nchini humo ni mbaya.
Barabara ambayo haijajengwa kwa kiwango cha lami, inaelezwa kuwa kikwazo
cha usafirishaji abiria na mizigo hasa nyakati za mvua.
Lakini, matumizi ya mipaka ya ziada kwa ajili hiyo yanatajwa kutumiwa vibaya na
watu wenye nia ovu kwa kupenyeza mbao zinazotokana na miti inayokatwa hovyo
mkoani Mtwara.
Mbali na mpaka halali wa Mtambasalwa, njia nyingine haramu zinazotumika
kupitishia mbao zinatajwa kuwapo kwenye eneo la mpaka unaokadiriwa kuwa na
urefu wa kilomita 130, kuanzia kwa wilaya ya Nanyumbu hadi Newala.
Usafirishaji wa mbao zilizovunwa kwa njia haramu unaelezwa kufanyika holela
pasipo kufuata taratibu, lakini hivi sasa uchunguzi wa kina unafanyika ili kubaini
chanzo (mahali zilipotoka).
Kumbukumbu za TFS, Kanda ya Kusini zinaonesha kuwa takwimu za matukio ya
watu waliokamatwa na mbao zinazodaiwa kutokana na uvunaji haramu ni za
mwaka 2012-2013 zikihusisha matukio 12.
Kati ya matukio hayo, mashauri tisa yanaendelea kwenye mahakama za mkoani
Mtwara wakati matano yakiwa yameshatolewa uamuzi uliowapa ushindi
walalamikiwa, ingawa Serikali imekata rufaani.
Hata hivyo, Mgiye amesema hujuma za usafirishaji mbao kwa njia haramu
kuziingiza Msumbiji na kuzirejesha nchini, zimedhibitiwa kupitia jitihada za pamoja
zinazotokana na vikao vya ujirani mwema kati ya pande mbili za Tanzania
(Mtwara) na Msumbiji (jimbo la Niasa).
Wajumbe wa vikao hivyo, kwa mujibu wa Mgiye ni Wakuu wa Kurugenzi wa
Wizara ya Maliasili na Utalii (Tanzania) na Wizara ya Ardhi, Mazingira na Misitu
kwa upande wa Msumbiji.
“Tuna vikao vya ujirani mwema vinavyofanyika mara moja kwa mwaka na
kupeana mbinu mbalimbali za kudhibiti vitendo hivyo,” amesema na kuongeza
kuwa mawasiliano kuhusu namna ya utekelezaji wa mipango ya udhibiti kati ya
pande mbili hizo yanafanyika mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mgiye, mipango hiyo ni pamoja na ufuatiliaji wa nyaraka muhimu
katika usafirishaji wa mazao ya misitu hasa mbao, ikizihusisha mamlaka za
mapato, lengo likiwa ni kubaini hujuma zinazofanyika.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Tanzania kuna vikosi vya kuzuia na
kupambana na uharibifu wa misitu ambavyo vimechangia kufanikisha udhibiti wa
biashara haramu hiyo.
Hitimisho
Ni dhahiri kwamba sekta ya misitu mkoani Mtwara ni moja ya rasilimali zenye
umuhimu wa pekee katika kukuza uchumi wa nchi, kuongeza pato la Serikali na
katika ngazi ya familia.
Lakini sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo ukataji miti
hovyo, unaosababisha kadhia kama uharifu wa mazingira na biashara haramu ya
mbao.
Hata hivyo, zipo jitihada zinazofanywa na mamlaka tofauti ikiwamo TFS kudhibiti
changamoto hizo, lakini haitoshi ‘kubweteka’, badala yake nguvu kubwa inapaswa
kuelekezwa katika mikakati ya kuifanya misitu kuwa endelevu.
Hitaji la kuendeleza jitihada za kudhibiti uharibifu wa misitu linapata nguvu kutoka
kwenye matukio yanayohusiana na uharibifu wa rasilimali ikiwamo ukataji miti
kwenye msitu wa Msanjesi.
Makala hii imeandikwa kwa ufadhili wa TMF.