SPIKA wa Bunge la Jamhuri wa Tanzania mstaafu, Mama Anna Makinda ametoa elimu wa uongozi wa Kijinsia kwa madiwani wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na TGNP Mtandao ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo madiwani hao. Akizungumza katika warsha hiyo, Bi. Makinda alisema suala la kuwajengea uwezo wanawake linapaswa kuanza mapema mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi ili kupata muda zaidi wa viongozi hao kupata elimu stahiki, kwani mara nyingi elimu hiyo hucheleweshwa kutolewa.
“…Kimsingi muda huu tumechelewa mikakati ya kuanza kumuwezesha kiongozi mwanamke hupaswa kuanza mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi hii itatusaidia hata kujipanga mapema uongozini…,” alisema Mama Makinda akizungumza na madiwani hao.
Aliwataka wanawake wote viongozi kuwa pamoja hasa wanapopigania masuala ya wanawake ili kwani umoja mara zote ni nguvu na utengano ni udhaifu. Changamoto za wanawake hazitofautiani kiitikadi za chama, rangi wala imani hivyo kuna kila sababu ya kuungana pale wanapogombea ajenda za wanawake.
Pamoja na hayo aliwataka madiwani wanawake kujipanga kimikakati na kutokubali kuondolewa katika nafasi za uongozi kizembe, kwani uwezo wa kuwatumikia wananchi wanao tena wa kiwango kikubwa kama watajipanga vizuri.
“…Hivi unakubalije mtu aliye nje kuja kukutoa katika nafasi yako kirahisi rahisi ilhali wewe upo karibu na wananchi, usikubali tuwaoneshe kwa vitendo tulioingia tusitoke kirahisi bila kupenda labda tupande ngazi lakini sio kushuka,” alisisitiza Mama Makinda.
Aidha aliwaomba kufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano na viongozi wa kiume kwani idadi yao ni kubwa hivyo ushawishi pekee ndio unaweza kuongezea nguvu ajenda zao. Alibainisha idadi ya madiwani na wabunge wa kiume ni kubwa ukilinganisha na wao hivyo njia pekee ya wao kufanikiwa ni kujenga urafiki, ukaribu na ushawishi kwa agenda anuai zinazobebwa na wanawake.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Bi. Suzan Lyimo akizungumza na madiwani hao aliwaomba kuwa kitu kimoja haswa wanapopigania masuala ya msingi kumuwezesha mwanamke.
Alisema kama wanawake hawatakuwa kitu kimoja hawawezi kufanikiwa katika agenda zao. Hata hivyo aliongeza kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kuanzia ndani ya vyama vya siasa kwani ndipo mipango mingi ya chama upangwa kwa utekelezaji zaidi.