Gumzo la kudai kuwa na muundo wa Serikali tatu haukuanza leo. Kwa wafuatiliaji wa mambo ya historia watakumbuka sakata la madai ya kuwa na serikali tatu yaliyoongozwa na Mbunge machachari wa Lupa enzi hizo, Njelu Kasaka, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam chini ya kivuli cha kundi lililojiita G 55. Waziri Mkuu mstaafu John Malecela anakumbuka kilichomsibu.

Sitaki kurudi huko, kila jambo lina historia yake. Leo katika makala haya nataka kuzungumzia athari za kuwa na serikali tatu na kufungua uwanja mpana wa mawazo kutoka kwa wazalendo na wapenda maendeleo ya kweli ya Tanzania.

 

Tatizo kubwa linalotusibu hapa nchini ni kutawaliwa sana na fikra za viongozi wachache ambazo siku zote hujiona wao ni miungu-watu, hivyo lolote watakalosema na kuamua litakubalika kirahisi kwa Watanzania ambao hawajui mustakabali wa taifa lenye kusifika kuwa na utajiri wa maliasili, unaoendelea kutafunwa na wachache kupitia mwanya wa uwekezaji.

 

Hivyo, kutokana na hili nadiriki kusema kuwa shinikizo la kuwa na serikali tatu halitoki kwa wananchi wa kawaida. Hawajui lolote kuhusu uendeshaji wa serikali hizi. Laiti wangejua na endapo wataendelea kuelimishwa kuhusu athari zake kiuchumi, ni matumaini yangu wengi hawatakubali kuunga mkono azimio hilo lililo katika Rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania 2013.

 

Miongoni mwa waumini wa serikali tatu ni Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba. Yeye binafsi, pamoja na wanatume wenye mtazamo kama huo wameamua kuingiza kipengele hicho kwa mada, ikiwa ni moja ya maoni ya wananchi walio wengi.

 

Mbona hawatwambii kwa kiwango cha asilimia. Kwamba miongoni mwa wanaohitaji muundo wa serikali tatu ni asilimia kadhaa kufuatia makusanyo ya mapendekezo katika pande zote za muungano.

 

Ninatambua kuwa rasimu ni andiko la awali ambalo halijafanyiwa marekebisho, na katika kufanya marekebisho ya rasimu kuna mambo makubwa matatu; mosi, kuondoa vipengele ambavyo vitaonekana haviungwi mkono na wengi kwa kupitia mabaraza na taasisi zilizoruhusiwa kisheria kutoa mapendekezo. Pili, kupunguza au kuongeza kipengele au vipengele katika ibara mbalimbali na, mwisho, kwa mtazamo wangu, ni kuvibakiza vipengele vitakavyoridhiwa na wengi vibaki kama vilivyo ili viingie kwenye katiba rasmi.

 

Sina uhakika juu ya mchanganuo wa masuala hayo. Kwa kuwa Tume ndiyo iliyopewa dhamana ina uwezo wa kuingiza kipengele ambacho si chaguo la wengi na kwa kuwa wengi miongoni mwetu tumekuwa wa kuyakubali ya viongozi, tutabaki tukisema “Liwalo na liwe”. Sasa huu si muda wa na liwalo na liwe. Ni muda mwafaka wa kutengeneza msingi imara wa nchi utakaoweza kusimamisha nyumba yetu kwa zaidi ya nusu karne ijayo.

 

Hivyo, endapo hili la serikali tatu litabaki kama lilivyo bila kurekebishwa au kuondolewa, Watanzania tutarajie au tuwe tayari kubeba mzigo mkubwa wa gharama za uendeshaji wa serikali tatu. Katika mfumo huu, serikali mbili zitawajibika kujiendesha na wakati huu kuiendesha serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kugharamia shughuli zote za kiserikali.

 

Mapato ya Tanzania Bara na Zanzibar, sehemu fulani itakuwa ikimegwa kwa ajili ya kugharamia serikali ya Muungano. Kwa kifupi watumishi wote wa Serikali ya Muungano kuanzia karani hadi rais, wataendesha maisha kwa gharama za mapato kutoka Bara na Visiwani, wakati huo serikali hizi mbili zitatakiwa kugharamia shughuli za maendeleo ya nchi zao zikiwamo za kuwalipa watumishi wa ngazi zote mishahara na marupurupu, na wakati huo huo, kufikiria namna ya kukusanya mapato ya kuboresha miundombinu mbalimbali katika nchi zao. Mathalani, elimu, afya, barabara, kilimo, ufugaji na mengine mengi.

 

Sasa tujiulize: Je, ni kweli mfumo huu mpya umekuja kumkomboa Mtanzania wa kawaida kutoka kwenye dimbwi la ufukara au ni mbinu mbadala ya wakubwa wachache kujitafutia fursa ya kulindana na kupeana ulaji?

 

Je, ni kweli pande zote mbili hizi za Muungano haziridhishwi na mfumo wa serikali mbili? Je, ni kweli kwamba kero na si matatizo ya Muungano kamwe hazitatatuliwa kwa mwendelezo wa mfumo tulionao sasa?

 

Je, maneno aliyosema Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere kuhusu ufa wa Muungano yanatimia?

 

Je, kwanini wanasiasa wachache waanze kulivalia njuga jambo hili bila kupima athari zake hapo baadaye, hususan katika nyanja zote za kiuchumi na kimaendeleo?

 

Nayasema haya kwa kuwa muundo huu wa serikali tatu tutarajie taifa kuingia gharama zisizo za lazima; mathalani kujenga ofisi mpya kwa ajili ya Rais wa Tanzania Bara na mawaziri wake, kwani hii iliyopo pale Dar es Salaam itabaki kuwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwani atakuwa jirani na wenzetu wa Zanzibar kimantiki.

 

Hivyo, rais na mawaziri wa Tanzania Bara ni lazima wajengewe ofisi katika Makao Makuu ya nchi mkoani Dodoma. Kama si hivyo, itabidi walipie majengo watakayokodi. Sasa sidhani kama rais ataishi na kufanya kazi kwenye majengo ya kukodi kama ilivyo desturi kwa mawaziri wapya wanapoteuliwa kushika nyadhifa zao.

 

Endapo rais atatumia Ikulu ndogo ya Dodoma nayo lazima itafanyiwa marekebisho iwe na hadhi ya rais wa Tanzania Bara.

 

Nasema hivi kwa sababu wote wanaowania kuingia Ikulu sasa hivi hawalali, wanakesha wakijiuliza swali kwamba endapo atagombea urais hekalu lake litakuwa wapi? Hicho bado ni kitendawili. Si kazi ya rasimu kubainisha hilo, litajulikana baadaye endapo hili halitabadilika kwenye rasimu.

 

Kwa mtazamo wangu, endapo hili litapita basi, haitakuwa busara kuwa na ofisi za Serikali ya Muungano na za Tanzania Bara katika mkoa mmoja. Lazima zitenganishwe ili kuleta taswira nzuri na ufanisi wa majukumu ya kiserikali.

 

Narudia kuweka msisitizo kwamba huu ni mtazamo wangu. Ukiachilia mbali suala la majengo, gharama nyingine ni za kuwalipa wanasiasa hawa. Unaweza kupunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri na watendaji wengine, lakini ukitumia mwanya huo kuwaongeza hawa wachache mishahara mikubwa na marupurupu tele kwa kisingizio kuwa wana mzigo mkubwa wa majukumu. Hili likifanyika katika serikali zote tatu, itakuwa ni sawa na kuruka majivu na kukanyaga moto.

 

Basi, napenda kutoa changamoto hii kwa watakaokuwa kwenye mabaraza na taasisi nyingine zitakazopata fursa ya kutoa maoni ya mwisho ili rasimu irekebishwe na kupata Katiba Mpya.

 

Sina tatizo na kuwapo serikali hizo tatu endapo hakutakuwa na mzigo utakaowalemea wengi kwa kisingizio cha kuepuka lawama za wachache, na wakati huo kuwafaidisha wachache kwa ama kuogopa kuuvunja Muungano, au kuepuka aibu iliyo mbele yetu.

 

Tutafute ujenzi wa taifa imara kama lilivyoachwa na waasisi wa taifa letu kwa kuleta Muungano wenye tija na maendeleo kwa pande zote mbili, bila upande mmoja kusononeka, hasa katika suala zima la uendeshaji serikali.

 

Tusitegemee fedha kutoka nje kuja kuendesha bajeti za serikali tatu. Wafadhili watawaunga mkono leo kwamba hili ni kukuza demokrasia, tutakapoanza kukwama katika bajeti zetu, ndipo utakapoona jeuri za wanaojiita wakubwa wa Ulaya na Marekani.

 

Tanzania ni nchi yetu, hatuna budi kutafakari kwa kina kila tunapotaka kufanya uamuzi mgumu kwa mustakabali kwa maendeleo ya taifa letu.

 

Pazia halijafungwa.

0763 400283

ericmanzi9@gmail.com