Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu ametoa miezi mitatu kwa wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 4 za fedha za halmashauri kwaajili ya kuwapa wanawake mikopo ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuunga mkono juhudi za serikali katika uchumi wa viwanda.
Amesema kuwa serikali haitasita kuwawajibisha wakurugenzi watakaokiuka maelekezo ya serikali yanayolenga kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais kwa wananchi ili kuwawezesha wanawake wa mijini na vijijini kiuchumi na hatimae kujiongezea kipato na kuwezesha uchumi wa viwanda.
“Linapokuja suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi hatutanii, chama cha mapinduzi tumepewa kura na wanawake wa Tanzania hasa wanawake wa vijijini na tumewaahidi wanawake kwamba tutawapa mikopo yenye masharti nafuu, kwahiyo pale ambapo mkurugenzi anashindwa kutenga fedha kwaajili ya kuwapatia wanawake mikopo hatutaelewana, na tunasubiri mpaka tarehe 30 June 2018 wakurugenzi wote ambao hawajatenga fedha na kuzitoa kwaajili ya wanawake tutapeleka majina yao kwa Mh. Rais Dk. John Pombe Magufuli,” Mh. Ummy alisisitiza.
Halikadhalika Mh. Ummy amepiga marufuku suala la kutoa fedha ndogo kwa kikundi kikubwa cha kinamama huku akitolea mfano kikundi cha watu sita kupewa 300,000 kuwa haitawasaidia kinamama hao katika juhudi za kujikwamua kiuchumi na kuongeza kuwa ni heri fedha hizo zikabaki kwa mkurugenzi ili ifanye shughuli nyingine lakini sio kuwakwamua kinamama.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuanza na maandamano yaliyotokea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa hadi katika Uwanja wa mpira wa Nelson Mandela akiwa ni mgeni rasmi wa sherehe hizo.
Awali akisoma risala Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura ameitaka serikali kuhakikisha wanafanya marekebisho ya sheria kinzani ili kuendana na mabadiliko ya mfumo wa maisha kama vile sheria ya ndoa, mirathi, maadili ya jamii na kiwango cha mchango wa mzazi katika malezi ya familia na watoto huku akitaja mafanikio kadha ya kufikia idadi ya asilimia 50 kwa 50.
“Kuanzishwa kwa vikundi na kuunganishwa na taasisi za fedha kama vile NMB, CRDB, Pride, SACCOS na SIDO kwaajili ya mikopo na vifaa kwaajili ya kufanyia kazi, pia mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri tumeweza kuwatambua wazee 48,732 wakiwemo wanawake na wanaume pia mkoa unaendelea kufuatilia masuala ya kijinsia dhidi ya watoto, jumla ya watoto 1,307 walifanyiwa ukatili na mashauri yao yapo polisi, dawati la jinsia na mahakamani,” Alisema.
Akichukua nafasi hiyo mbunge wa Sumbawanga Mjini Mh. Aesh Hilally nae alimuomba Mh. Ummy kuona umuhimu wa kuongeza gari za wagonjwa nae Mh. Ummy alikubali ombi hilo na kuahidi kutoa gari za wagonjwa mbili, moja ikihudumia hospitali ya rufaa ya mkoa wa rukwa na nyingine katika kituo cha afya kilichopo manispaa ya Sumbawanga.