Soko la Kampochea lililopo Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam limeteketea kwa moto alfajiri ya leo Jumanne Machi 6, 2018 na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Imeelezwa moto huo ulianza kuteketeza mabanda ya soko hilo saa 12 alfajiri huku uongozi ukitaja kuwa chanzo ni hitilafu ya umeme.
Mwenyekiti wa soko hilo, Mohamedy Njiwa amesema limekuwa likikumbwa na hitilafu za mara kwa mara licha ya kuripoti kwa mamlaka husika.
“Wiki mbili zilizopita hapa kulikuwa na hitilafu ya umeme, ulikuwa unakuja na kukata. Tanesco walikuja kufanya ukaguzi wakaeleza kuwa kuna hitilafu kwenye transfoma,”amesema.
Amesema mabanda yote 673 yaliyokuwapo eneo hilo yameungua kwa moto na kwamba, hasara ni kubwa.
Mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, Chacha Mwang’wene amesema hajafanikiwa kuokoa chochote zaidi ya taarifa zake za biashara.
Msemaji wa Zimamoto Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Peter Mwambene amesema jeshi hilo lilijitahidi kudhibiti moto huo, lakini tatizo kubwa ni aina ya bidhaa zilizokuwamo.
“Soko hili lina mali ambazo zinachangia kusambaza moto kwa kasi sana kama mitumba ambayo ni rahisi kuteketea kwa moto,”amesema.
Pia, amesisitiza kuwapo kwa vifaa vya awali vya kuzimia moto ili kunusuru mali kwenye masoko mengine jijini hapa.
Hatahivyo, wafanyabiashara hao wameeleza nia yao ya kuendelea kulitumia soko hilo licha ya agizo la mkuu wa Wilaya ya Temeke kuwataka kuhamia masoko mengine.