Mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi wa Tanzania (TSNP), Abdul Nondo, akiongea na waandishi wa habari leo.
Ndugu waandishi wa habari, leo tunapenda kutoa ufafanuzi kidogo juu ya tuhuma zilizotolewa na TAHLISO dhidi ya TSNP mnamo tarehe 3/3/2028.

Taasisi yetu ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyosajiliwa tarehe 23/10 /2001.  Lengo kubwa ikiwa ni kutetea wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu na kuwapa utambuzi watambue na kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Ndugu waandishi wa habari, tumekuwa tukishirikiana na wizara ya elimu ambapo Waziri wa Elimu, Mh. Dkt. Ndalichako, Naibu Waziri, Ole Nasha, pamoja na Naibu Katibu wa wizara hiyo, Dkt.  Ave Marie Semakafa wamekuwa wakitusaidia kutatua changamoto za wanafunzi vyuo tofauti-tofauti kama vile MWECAU, CBE, ARDHI na MZUMBE.

Pia, tumekuwa tukishirikiana na taasisi mbalimbali za kiserikali katika utatuzi wa matatizo ya wanafunzi nchini. Kwa mfano, tumekuwa tukipata ushirikiano mzuri kutoka bodi ya mikopo wanafunzi wa elimu ya juu nchini kuhusiana na mchakato wa utoaji mikopo.
Pia tumekuwa tukishirikiana na tume ya vyuo vikuu nchini ( TCU) katika kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika suala zima la udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Wanafunzi wa Pugu tumeshirikiana nao vizuri sana.

Na vilevile tumekuwa pia tukitumia vyombo vya habari kutoa mapendekezo yetu, kuelimisha wanafunzi na hata kuwajulisha watendaji wa serikali kuhusiana na uwepo wa tatizo mbalimbali kuhusu wanafunzi.

Lakini jambo la kushangaza mbali na kutimiza wajibu wetu kisheria, TAHLISO iliamua kwa makusudi kutushambulia bila kuwa na hoja zozote zile za msingi.

Tukumbuke kuwa TSNP haifadhiliwi na mtu yeyote wala taasisi yoyote ile, lakini tumekuwa mstari wa mbele kuwa sauti ya wanafunzi nchini.

TAHLISO ambayo kila chuo kikuu nchini kinatoa ada isiyopungua shillingi laki tano kwa mwaka ili TAHLISO iweze kutetea maslahi ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, imeacha kutimiza wajibu wake wa msingi na badala yake imegeuka kuwa taasisi yenye kusema kwa niaba ya serikali pamoja na kushambulia taasisi ambazo zinatetea maslahi ya wanafunzi nchini ikiwemo TSNP.

KUHUSU KIFO CHA AQUILINE

Ndugu waandishi wa habari, marehemu Aquiline alikuwa na haki zake za msingi kama binadamu ikiwemo haki za kuishi,na kila taasisi au mtu yeyote ana haki ya kukemea matendo yeyote maovu dhidi ya binadamu.
Tuwaulize TAHLISO, wao wanapata wapi mamlaka ya kukataza, kuonya, kukemea makundi, watu,taasisi zilizoguswa na suala hili kusemea juu ya tukio lile?

Pili, Aquiline alikuwa ni mwanafunzi pia, TSNP ni mtandao wa kutetea wanafunzi, tunayo hayo mamlaka kusemea, kukemea, kushauri na hata kutoa mapendekezo yetu juu ya tukio lolote linaloashiria upotevu wa haki kwa wanafunzi.  TAHLISO wanatoa wapi ujasiri, mamlaka ya kutuzuia TSNP tusitimize wajibu wetu?

Tatu, TSNP tumekuwa mstari wa mbele kusemea shida za wanafunzi mikopo, udahili, wanafunzi kufukuzwa na tumeshirikiana na taasisi za serikali na hata viongozi wa serikali katika utatuzi wa shida za wanafunzi, TAHLISO inayojinasibu kuwa inatetea wanafunzi ije iseme ilifanya nini kati ya haya hadi leo iwe na ujasiri na mamlaka ya kushambulia TSNP.

 

KUHUSU TSNP KUTUMIWA NA WANASIASA

Ndugu waandishi, TSNP ni taasisi ambayo haifungamani na chama chochote kile cha siasa na haifanyi kazi ya chama chochote.
Na ndiyo maana mara zote mmekuwa mkituona huwa tuna agenda zinazohusu wanafunzi tu kama vile mikopo ya wanafunzi, udahili wanafunzi, mmetuona katika makongamano ya wanafunzi.
Pia tulitoa maoni na mapendekezo yetu kuwa kama hatua stahiki hazitachukuliwa Mh. Mwigulu ajiuzulu (individual ministerial responsibility) kutokana na matendo dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu kushamiri bila kuwepo kwa taarifa juu ya uchunguzi na hatua stahiki kwa wahusika.
Lakini jambo la kushangaza TAHLISO wametoka mbele kutetea serikali na wizara ya mambo ya ndani na kuacha jukumu la kuwatetea wanafunzi.
Inashangaza sana kuona TAHLISO inaishambulia TSNP na kudai kuwa inatumiwa kisiasa ilihali tunashughulika na shida za wanafunzi, na wao wamejisahau wanavyoshughulika na majukumu ya kusemea na kutetea serikali.

Kwa mantiki hii sasa, kama TAHLISO wanatulaumu na kutushambulia, wanatushambulia na kwa lipi?

HITIMISHO

Tunawataka TAHLISO waache kuwa wasemaji wa wizara na serikali na wakumbuke majukumu yao mazito ya kusemea wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu wanalipishwa ada vyuo vikuu.
Hivyo kulipishwa ada pasipo kutimiza wajibu unaotakiwa kutimiza, hiyo ni silent corruption.

Imetolewa na:
Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP)