WIKI iliyopita Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alitangaza bajeti ya mwaka 2012/2013. Nafahamu kuwa mpendwa msomaji umeishasoma mengi kuhusiana na bajeti hii. Kwa mantiki hiyo mimi sitajielekeza katika kuchambua nini kimeongezwa kodi au kupunguzizwa kodi kama ulivyo utamaduni wa makala nyingi.

Tunafahamu sote sasa kuwa bajeti hii ya shilingi trilioni 15 na ushehi hivi, imekuwa ya ujumla mno. Bajeti hii sikuiona kama inalenga kutatua tatizo la njaa, umeme, barabara mbovu, reli, viwanja vya ndege, elimu, afya au hata mahusiano ya jamii. Kiwango kilichotengwa nadiriki kukiita umwagiliaji wa matone (drip irrigation).

Hata Waziri Mgimwa aliyeisoma bajeti hii kwa mara ya kwanza maishani mwake, naamini hadi leo yupo kwenye mshangao. Hajasikia mshindo. Hakuna jipya lililotokana na tangazo lake la bajeti. Labda hizo Sh milioni 50 anazotarajia kupata kutokana na matajiri wenye kuweka majina yao kwenye magari binafsi. Kwa bahati mbaya ingetokea mimi ndiye Waziri wa Fedha, nchi hii ningeishitua mbavu.

Sitanii, mzee huyu Dk. Mgimwa tulikutana pale Ikulu siku anaapishwa na ilikuwa hatufahamiani ila nilizungumza naye na niliona ni mtu mwenye mwelekeo fulani wa kulisaidia taifa hili, ila pamoja na upya wake katika wizara hii, ambako hajamaliza miezi miwili kamili, nilitarajia angefanya jambo la kuwafanya Watanzania watambue ujio wake.

 

 

 

Yapo mambo ambayo yanahitaji uamuzi tu. Kwa mfano. Hivi ninavyoandika makala hii, Serikali inamiliki magari yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 5. Magari haya wala hayana manufaa yoyote kwetu sisi wadau na wananchi. Wala haya magari si mabasi ya abiria kama daladala au ilivyokuwa Kamata zamani au idadi hii haijumuishi magari ya UDA.

Magari haya ni mashangingi, Benz, BMW, RAV4, na magari mengine mengi ya starehe. Katika orodha hiyo hakuna hata magari ya kubebea wagonjwa. Kama mimi mwongo yaangalie magari ya kubebea wagonjwa (ambulance). Mengi namba zake zimeandikwa DFP. Maana yake yametolewa na wafadhili. Sijapata kuona ambulance iliyoandikwa STK. Aliyeiona tafadhali anisaidie.

Hii ina maana magari haya tunayoyalipia asilimia 33 ya bajeti kuu ya Serikali, wala hayatuasaidii. Imefika mahala magari ya serikali tuliyonunua kwa fedha zetu, baadhi ya watumishi wahuni wanayabandika makaratasi ya tinted na kuyatumia kutongozea wanawake/wanaume. Magari haya yanarandaranda baa hadi usiku wa manane.

Pinda mzee wa chondechonde, anaihadaa jamii yetu. Eti mzee yule anayejidai sasa amegeukia ufugaji nyuki, anawambia watu anakerwa na mashangingi lakini yeye anayapanda. Novemba mwaka jana, nilikuwa India katika jiji la Bangalore. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa India, Somanahalli Mallaiah Krishna (nilipiga naye picha baada ya kuvutiwa hili) ambaye kwa hadhi yake ni kama Waziri Mkuu wa hapa anatumia Toyota Corolla E 100.

Ukiacha vipuri tu, Corolla inatumia wastani wa lita moja ya mafuta kwa kilomita 12 hadi 14. Haya mashangingi tunayoyaona barabarani mengi yanatumia wastani wa lita moja kwa kilomita 6. Tena mengine yanatumia hadi lita 4 kwa kilomita. Matengenezo ya magari haya tofauti ni dunia na mbingu. Corolla ukifanya service ya 200,000 gari lenyewe linashtuka. Kwa shangingi kiasi hicho kinanunua filter tu. Shangingi ukifanya service ya Sh 2,000,000 unaacha deni la 1,500,000 gereji!

Nasema katika eneo hili pekee tunachoma moto uchumi wetu si chini ya asilimia 40 ya pato halisi. Moja ya matarajio yangu kwenye bajeti hii na jambo ambalo ningelifanya kama ingetokea mimi nikawa Waziri wa Fedha, basi mara moja ningefanya walichofanya Kenya na Rwanda. Ningefuta utaratibu wa Serikali kumiliki magari.

Ningeanzisha Sera ya kila mtumishi mwenye haki ya kupewa gari kwa sera ya sasa, basi akopeshwe gari moja kwa moja. Ikibidi wala nisingezunguka. Kila aliye na gari hilo hilo ndilo ningeanzia kumkopesha. Kwa macho yangu nimeshuhudia watumishi wanaokwenda baa wakaacha gari inawaka na kiyoyozi kuanzia saa 11 jioni hadi saa 8:00 usiku wanapotoka baa. Usishangae ni kweli, wala sijatia chumvi.

Bosi ambaye kwa sasa gari likipata mafua tu analipeleka CMC, akilimiliki yeye litatengenzwa mwembeni na bado mambo yatakwenda. Dereva ambaye alikuwa anweza kuuza betri, tairi mpya zilizofungwa na Serikali akapachika spea mbovu, hatafanya hivyo kwa bosi anayenunua tairi kwa kutegemea mshahara. Uratibu utakuwa wa karibu mno. Baada ya uamuzi huu ningewapa wastani wa Sh 300,000 kila afisa kwa ajili ya mafuta. Nina uhakika ningeokoa wastani wa Sh 2,000,000 kama gharama za kuendesha gari moja kila mwezi.

Pili ningeamua kufanya uamuzi wa ukichaa. Hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na umeme wa uhakika. Kwamba mradi kama wa umeme wa Mradi wa Stiglers Gorge wenye uwezo wa kuzalisha umeme hadi megawati 3,000 ningeutengea robo ya fedha za bajeti yetu yaani Sh trilioni 3.5. Ebu kwa akili ya kawaida angalia mijini na vijijini uone tofauti kubwa iliyopo kati ya eneo lenye umeme na eneo lisilo na umeme.

Nchi hii tukiwa na umeme wa kutosha wawekezaji watakuja wenyewe. Hawa wakiishajenga viwanda, watajenga barabara wenyewe. Nchi kama Uingereza zimefanya hivyo. Barabara nyingi zimejengwa na watu binafsi. Enzi za Enclosure System, matajiri akina Rotterdam na Meticalf walijenga wenyewe barabara na Serikali ikarejeshewa barabara hizo baada ya muda chini ya utaratibu wa Build Operate and Transfer (BOT).

Leo sisi tunahangaika na kupunguza ushuru kwa asilimia 10 bila kuweka uwekezaji wa maana kwenye umeme. Nchi hii kwa ukubwa wake tunapaswa kufikiria kuwa na umeme megawati 20,000. Leo hiki kibaba cha megawati 500, tunajidanganya. Nani aje kuwekeza kwenye nchi yenye umeme wa kutegemea majenereta. Tunayo mito, gesi na urani ya kutosha, hapa ulipaswa kufanyika uamuzi wa ghafla tukazalisha umeme wa kutosha na tukavuna.

Sitanii, yapo maeneo ya kupata fedha za bure. Leo tunaambiwa deni la taifa limeruka kutoka Sh trilioni 14 kwenda 22, lakini Serikali kwa kuchekacheka tu viongozi wake wanasema utafikiri ni sifa. Hawasemi deni hilo limetumika kufanya nini. Yaani Mwalimu Julius Nyerere ameongoza nchi hii kwa miaka 23 hakuacha deni hata la trilioni 2, leo Dk. Jakaya Kikwete ameendesha miaka saba tu, tena hili tatizo linatajwa kuanza 2009 baada ya Richmond, amerusha kutoka trilioni 14 hadi 22 kwa miaka miwili tu? Tunataka maelezo kama Watanzania.

Nasema nchi yetu ingeweza kuchukua mkopo hata wa trilioni 10, tukajenga reli ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Kampala, Kinshasa, Lubumbashi, Ndola, Kitwe, Lilongwe, Kigali na Bujumbura. Kwa uamuzi huo tu, bandari ya Dar es Salaam ingepanuliwa hadi mwambao wa Tanga. Mizigo itasafirishwa saa 24 tukawa tunavuna ushuru wa kutumia bandari na reli yetu.

Makusanyo haya yangetuwezesha kupumzika kama taifa. Tungepata mamilioni ya dola, tukalipa deni lenyewe na kuacha kutegemea misaada ya wahisani.

Sitanii. Leo nchi yetu imefika pahala hatuna mwelekeo? Tumeona kimbilio pekee ni kuongeza kodi kwenye soda, mvinyo na bia. Hivi nchi hii bila kuamua kufanya uwekezaji mkubwa kama wa umeme na usafirishaji kisha tukaondokana na umiliki wa magari kwa Serikali unadhani ipo siku tutaondokana na umasikini? Ndugu zangu Watanzania. Labda tuzikiri uchi.

Sitaki kuwahamasisha Watanzania, lakini anzeni kufikiria. Najua hakuna serikali yoyote milele inayoweza kugawa fedha kama njugu bila watu kufanya kazi. Hata hivyo, ni jukumu la Serikali kuweka sera na mipango mizuri. Mipango hii ndiyo yenye kutuwezesha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kuushinda umasikini.

Inavyoelekea hawa wametuchoka. Tukilibaini hilo, nasema si vyema kuendelea kuwaonea aibu. Yatupasa sasa kuanza kuandaa shahada zetu za kupigia kura, kisha wakati mwafaka ukifika tuzitumie vyema kuleta mabadiliko katika nchi hii. Chonde usimpige mtu ngumi, ila jiandae kumnyima kura asiyekuletea maendeleo. Hatuwezi kuendelea kwa bajeti za kodi za soda na bia.

Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa +255 (0) 784 404827 au [email protected]