Watu 79 wamekufa baada ya paa la klabu moja maarufu ya usiku katika Jamhuri ya Dominika kuporomoka. Miongoni mwa waliokufa katika tukio hilo la usiku wa manane ni mwanasiasa mmoja na mchezaji nyota wa Baseball.

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa Merengue nchini Dominika Rubby Perez, ambaye alikuwa jukwaani wakati huo, ni miongoni mwa watu waliojikuta kwenye mkasa huo uliotokea katika klabu ya usiku ya Jet Set kwenye mji mkuu wa taifa hilo la Caribbean wa Santo Domingo.

Saa chache baada ya paa hilo kuanguka, alikuwa bado amekwama pamoja na wengine, wakati zaidi ya waokoaji 370 wakipekuwa kwenye vifusi na waathiriwa walionasa wakiomba msaada. Vyombo vya habari nchini humo vilisema alipatikana akiwa amekufa. Kulikuwa na kati ya watu 500 na 1,000 katika klabu hiyo wakati mkasa ulipotokea mwendo wa saa saba kamili usiku wa manane. Haijajulikana kilichosababisha paa hilo kuporomoka.