TASAC kuhakikisha huduma za usafirishaji kwa njia ya maji zinakuwa bora

Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa limejidhatiti kuhakikisha huduma za usafirishaji kwa njia ya maji zinatolewa kwa ubora, ufanisi na kwa wakati.

Aidha TASAC imetoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na fukwe au maziwa wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama ili kudumisha usafiri kwa njia ya maji.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nelson Mlali alipozungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane-Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema mojawapo ya kazi za TASAC ni kusimamia sekta ya usafiri kwa njia ya maji, ambapo wana jukumu la shughulika na meli pamoja na mizigo.

“Tumepokea changamoto katika Makundi mbalimbali ikiwemo viwango mbalimbali vya tozo katika mnyororo wa usafirishaji mizigo yao kwa njia ya bahari, ucheleweshaji wa meli kupata eneo la gati, uchelewaji wa magari katika mipaka yetu ambayo yanachukua mizigo bandarini na kwenda nchi jirani.

“Kwahiyo sisi tutakachokifanya ni kukutana na wadau wetu ili kujaribu kuangalia namna bora ya kuweza kupunguza tozo ili kuzifanya bandari zetu zisiwe ghali kutumika kwa wananchi na tuweze kumudu ushindani katika bandari zetu na kuhakikisha huduma za usafirishaji zinatolewa kwa ubora na ufanisi,” amesema.

Ametoa wito kwa wananchi Watanzania wajitahidi wanapoina TASAC waende ili waweze kupata elimu pamoja na suluhisho la changamoto wanazozipata wanapotumia usafiri wa maji.

“Lakini vilevile tunaomba ushirikiano wao hasa wale walio karibu na maji, Pwani za bahari, fukwe au maziwani wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanakuwa salama ili kudumisha usafiri kwa njia ya maji,” amesema.

Akizungumzia ushiriki wao katika maonesho hayo, amesema Wakulima na Wafugaji ni wadau muhimu katika kusafirisha mizigo yao kupitia njia ya maji.

“Na niwaambie kwamba zaidi za asilimia 90 ya mizigo inayosafirishwa inatumia njia ya maji, kwahiyo umeshaona TASAC tunavyohusika katika maonesho haya,” amesema.

Amebainisha kuwa, Tanzania inasafirisha mazao ya Kilimo ya aina mbalimbali ikiwemo Kakao, tumbaku pamoja na Zabibu.

“Katika suala la mifugo pia tunahusika kwa wale wanaosafirisha mifugo hai na tunasafirisha kwa wingi wanyama hai kwenda Comoro. Kwahiyo TASAC inahusika kukagua meli zile lakini pia inahusika kuangalia hiyo mifugo mpaka ifike salama.

“Kwa upande wa uvuvi pia wanatumia vifaa vya aina mbalimbali, sisi tunahusika pia kukagua vyombo vyao kwa maana ya usalama na kuvipa leseni. Kwahiyo unakuta kwamba katika mnyororo wa shughuli hii TASAC inahusika,” amebainisha.

Please follow and like us:
Pin Share