Jumla ya watu 601 wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalum iliyokuwa ikifanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).
Kambi hiyo ya siku tano iliyoenda sambamba na utoaji wa mafunzo ya kutumia mashine ya kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – Echo) kwa wataalam wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa imemalizika leo ambao watu wazima 571 na watoto 30 wamepatiwa matiabu ya moyo huku tatizo kubwa lililoonekana kwa watu wazima likiwa ni shinikizo la juu la damu.
Akizungumza na waandishi wa habari Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallagyo alisema wametoa rufaa kwa wagonjwa 80 waliohitaji uchunguzi zaidi na wale waliohitaji upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo kwenda JKCI kwa ajili ya kupatiwa matibabu hayo.
Dkt. Pedro amesema watu wazima wengi waliofanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo wamekutwa na magonjwa ya shinikizo la juu la damu, magonjwa ya mishipa ya moyo kuziba na magonjwa ya valvu za moyo kuziba au kuvujisha damu kwenye moyo.
“Asilimia 56 ya watu wazima waliofanyiwa vipimo vya moyo walikutwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, utafiti tulioufanya tumeona wagonjwa hawa hawapo katika matumizi mazuri ya dawa, bado kuna ule uelewa mdogo wa kwamba dawa za presha zinatumika kwa muda mfupi na mtu anavyojisikia vizuri anaziacha hivyo kuleta matokeo mabaya yanayoweza kusababisha matatizo ya figo, uoni hafifu, kiharusi na matatizo mengine”, amesema Dkt. Pedro
Upande wa watoto Dkt. Pedro amesema wamewapa rufaa watoto 16 waliokutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ambapo watoto watano walikuwa na magonjwa ya moyo waliyoyapata baada ya kuzaliwa yaani moyo kutanuka na valvu kutokufanya kazi vizuri.
“Watoto wengine 11 tuliowapa rufaa ni wale wenye magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu, mishipa mikubwa inayotoa damu kwenye moyo kupeleka mwilini na kwenye mapafu kupishana hivyo kuhitaji rufaa ya haraka kufika JKCI kwa ajili ya upasuaji wa moyo”, ame.sema Dkt. Pedro
Dkt. Pedro amesema watoto walioonwa katika kambi hiyo na kupewa rufaa wengi wao walikuwa katika hali mbaya hivyo kuhitija kusafirishwa haraka kwenda Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) Dkt. Alfred Mwakalebela amewapongeza wataalam wa JKCI kwa kufanya kazi kwa kujituma kuwahudumia wananchi wa Iringa kwa upendo.
Dkt. Mwakalebela alisema kupitia kambi hiyo wameweza kupata maono yanayoonyesha ukubwa wa matatizo ya moyo kwa wananchi wanaowahudumia kwani hapo awali hawakujua kama uhitaji wa tiba ya moyo kuwa mkubwa kama ambavyo imeonekana katika wiki ya moja ya matibabu hayo.
“Watu wa Iringa wana hamu sana ya kujua afya zao naomba muendelee kuja Iringa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wetu kwani bado wanayo kiu ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Mwakalebela
Naye Afisa Lishe Kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji alisema asilimia 60 ya watu waliojitokeza kupimwa moyo walikuwa na uzito uliopitiliza hivyo kuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
“Matokeo haya tumeyapata baada ya kufanya kipimo cha uwiano kati ya urefu na uzito pamoja na kipimo cha kuangalia mzunguko wa mafuta kwenye eneo la tumbo na kuwakuta watu wengi na uzito mkubwa pamoja na viriba tumbo”, alisema Husna.
Husna alisema uandaaji wa vyakula vya nafaka pamoja na ulaji wa vyakula hivyo katika Mkoa wa Iringa inaweza kuwa sababu ya watu wengi kupata uzito uliopitiliza jambo ambalo kiafya si zuri.
“Watu wengi walioshiriki katika zoezi la upimaji huu wametuambia kwamba uandaaji wa unga wa ugali ujulikanao kwa jina la Kiverege ambao mahindi uoshwa, kukobolewa, kusagwa na baadaye kuanika tena unga ule kwa siku tatu hadi nne hivyo kuondoa virutubisho vilivyopo katika mahindi”,
“Upatikanaji na ulaji wa mboga za majini katika Mkoa huu uko vizuri lakini changamoto inakuja kwenye uandaaji wa mboga hizo kwani zimekuwa zikipikwa kwa muda mrefu hivyo kupoteza virutubisho vyake”, alisema Husna.