pg 1Watanzania wanaotegemea usafiri wa meli katika maziwa ya Victoria, Nyasa na Kigoma wako njia panda baada ya meli karibu zote zilizokuwa zinafanya kazi kuharibika.

 Ukiacha meli kuharibika, wafanyakazi wa Kampuni ya  Marine Services Co. LTD (MSCL), inayoendesha huduma za usafiri majini katika maziwa mbalimbali nchini chini ya Serikali, hadi sasa hawajalipwa mshahara kwa miezi mitano, uchunguzi wa JAMHURI umebainisha.

Kutokana na ukosefu wa mishahara, wafanyakazi wameanza kushikana uchawi kwa kuona wapo watu wanaofaidika kwa mgongo wao au kulindwa na vigogo wenye dhamana na uendeshaji wa huduma ya usafiri wa majini huku wakisema, huduma hii imetelekezwa.

 “Hili ni suala linalohitaji kupatiwa majibu ili Umma wa Watanzania wanaotegemea huduma ya usafiri wa majini na Wafanyakazi wa Kampuni hii waweze kujua hatima yao, ikiwamo suala la ukosefu wa mishahara kwa miezi minne sasa,” anasema mmoja wa wafanyakazi aliyezungumza na JAMHURI huku akionyesha nyaraka.

 Wafanyakazi wameliambia JAMHURI kuwa kwa sasa hakuna huduma zilizokuwa zinatolewa na Kampuni hiyo, kampuni hiyo inajishughulisha na usafirishaji wa mizigo na abiria kwa kutumia meli katika maziwa makuu; yaani Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

 Tangu enzi za iliyokuwa Jumuia ya Africa Mashariki (EAC), kampuni hiyo ilikuwa ni idara chini ya Shirika la Reli. Na hata baada ya jumuia kuvunjika, kitengo cha meli kilibakia kuwa idara ndani ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), anasema mmoja wa wafanyakazi.

 Wanasema, hali iliendelea hivyo hadi mwaka 1999 Serikali ilipoiondoa idara hii kwenye shirika la reli na kuifanya kuwa ni kampuni inayojitegemea kwa jina la Marine Services Co. LTD (MSCL) ikiwa ni mali ya Serikali kwa asilimia 100.

Wakati inaanzishwa kama kampuni kutoka TRC, wanasema haikupewa hata senti moja kutoka TRC, lakini ilianzishwa na mali zake zote. Mali hizo ni pamoja na meli, bandari zote katika maziwa makuu, karakana na mashine zake zote, vyelezo vya meli ( floating docks kwa Ziwa Victoria – (02) na Slip way kwa Ziwa Tanganyika – (01) ), Majengo (yaani: Ofisi, Ghala za kutunzia mizigo, mabanda ya kupumzikia abiria, stoo za vipuli pamoja na vipuli vilivyokuwepo, magari, trekta) n.k. Angalau mpaka hapo hali haikuwa mbaya kwani vyombo vyote vya MSCL vilikuwa havijachakaa na uwepo wa vipuli na karakana ilikuwa ni uhakikisho wa huduma kuendelea vizuri.

 Wanasema tatizo lilianza mwaka 2006 ambapo Serikali ilihamisha sehemu kubwa ya mali za kampuni kutoka MSCL kwenda TPA (Tanzania Ports Authority). Mali wanazosema zilihamishiwa TPA ni pamoja na bandari zote, majengo yote, vyelezo vyote vya meli, maghala ya mizigo, majengo ya kupumzikia abiria, stoo za vipuli na hata vipuli vya meli, baadhi ya magari na trekta. MSCL ilibaki na meli tu maelekezo yakiwa kwamba MSCL:

1. Ilipe mishahara ya wafanyakazi

2. Igharamie matengenezo madogo ya meli; na

3. Iwajibike na gharama zote za uendeshaji wa ofisi na meli.

 Wajibu wa Serikali kwa kampuni ilikuwa ni kugharamia matengenezo yote makubwa (major overhaul ) kwa injini, jenereta na vinyakuzi. “Bahati mbaya kwa MSCL, mpaka leo ni meli moja tu ya MV Umoja ndiyo imewahi kupata bahati ya kufanyiwa matengenezo makubwa kwa pesa ya Serikali mwaka 2012/2013. Meli nyingine zote hazijawahi kupatiwa huduma ya matengenezo makubwa, matokeo yake ni kuwa meli na mitambo yake zimechakaa kupita kiasi hali inayosababisha meli kutokuwa salama kwa usafirishaji wa majini na hivyo SUMATRA kuwa inatoa tamko la kuzisimamisha hali ya uharibifu inapozidi,” ameliambia JAMHURI mfanyakazi mwingine.

Wanasema meli zilizosimamishwa na SUMATRA kwa muda mrefu mpaka sasa ni: MV Victoria, MV Butiama, MV Iringa, MT Ukerewe, Serengeti, ML Wimbi na ML Maindi. Kusimama kwa meli hizi, ina maana wananchi waliokuwa wanapata huduma ya bei nafuu kwa sasa wanalazimika kutumia mabasi.

 Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa hata hizo zilizopo zinafanya safari zake kwa kusuasua kwa kuharibika mara kwa mara. Meli zilizopo ni MV Liemba, iliyopo Ziwa Tanganyika, MV Clarias, MV Songea iliyopo Ziwa Nyasa na MT Sangara.

“Serikali imekuwa inaonekana kujali panapokuwa na matatizo kwenye meli yanayotishia usalama wa raia na mali zao, hapo ndipo tume huundwa haraka haraka na kutoa mapendekezo ambayo huwa hayafanyiwi kazi. Vinginevyo, viongozi wakuu kutoka wizarani (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ) wamekuwa wakifanya ziara kwenye kampuni kama Watalii.

 “Wakija hufikia hotelini, wanazungushwa na magari ya MSCL hata katika ratiba za kukagua na kutembelea shughuli za taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hii. Wakitembelea MSCL, huzunguka kwenye meli na kuishia makao makuu na kufanya vikao na menejimenti tu. Hawajawahi kufanya vikao kwa kuzungumza na wafanyakazi kwa muda mrefu pamoja na hali mbaya ya kampuni kwa sasa.

“Hivi sasa hali ni tete sana MSCL, wafanyakazi tuna miezi minne hawajalipwa mishahara na wala haijulikani kuwa hatima yetu itakuwaje. Tumekuwa ni wahanga kwa maamuzi yanayotolewa na Serikali! Baadhi ya hospitali zinakataa kutupa huduma za matibabu ingawa kampuni ina mkataba na NHIF. NHIF inatoa sababu kuwa tangu mwezi Julai 2015, MSCL haijawasilisha michango ya wafanyakazi ilhali wafanyakazi wamekuwa wakikatwa kila mwezi ukiondoa hii miezi ambayo wafanyakazi hawajalipwa Mishahara,” anasema kwa uchungu mfanyakazi mwingine.

 Taarifa zinaonyesha kuwa wastaafu pia wanapata shida kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii (PPF na NSSF), inakonekana kuwa mwajiri amekuwa hawasilishi michango ya wafanyakazi kwa wakati.

 Wanalalamika pia kuwa mfumo wao wa ajira umebadilishwa kutoka mfumo rasmi wa watumishi wa Taasisi za umma na kuwa mfumo usio rasmi wa ajira katika taasisi zilizosajiriwa nchini zisizo za Serikali! “Uthibitisho juu ya hili unaonekana baada ya wastaafu kuambiwa kuwa mwajiri anawajibika kuwapa nauli tu ya kuwafikisha makwao bila kulipwa kiinua mgongo kama ilivyo kwa watumishi wa Serikali Kuu na waajiriwa katika mashirika na kampuni myingine za Serikali.

 “Hali hii ni tofauti na ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa kwa TPA katika maziwa makuu na MSCL kupokonywa assets (mali) zake. Mstaafu wa MSCL analipwa nauli tu na kuambiwa afuatilie michango yake kwenye ofisi za mifuko ya jamii, hakuna cha mkono wa kwa heri wala kingine chochote,” anasema mfanyakazi mwingine aliyeko Bandari ya Mwanza.

 Mfanyakazi mwingine aliyeko Bandari ya Kigoma, ameliambia JAMHURI kuwa wafanyakazi hawalipwi madai yao kwa kisingizio kuwa kampuni haina pesa, ilihali wadai wa nje madeni yao hushughulikiwa na kuombewa pesa serikalini na kulipwa.

Hayo yakiendelea, mameneja wamekuwa wakiendelea na safari za mara kwa mara zisizokuwa na mrejesho. Manejimenti iliyopo kwa sasa inatajwa kuwa haijawahi kufanya kikao na wafanyakazi hata mara moja kueleza hali halisi ya kampuni na nini kinachotarajiwa.

 Wanasema Bodi ya MSCL imekuwa inafanya teuzi za wakuu wa Idara pasipokuzingatia sifa za Kitaaluma wala uzoefu. Wanataja uteuzi wa Mkuu wa Idara ya Masoko na Biashara (Idara ambayo ni uti wa mgongo kwa uhai na ustawi wa Kampuni) kuwa hana sifa za kitaaluma katika fani hiyo.

 Wanahoji inakuwaje mtumishi mwenzao amepandishwa cheo kuchukua nafasi ya Meneja Mkuu aliyewajibishwa kwa kusimamishwa kazi baada ya kudaiwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za Serikali kwenye mradi wa matengenezo ya Meli ya MV Victoria, ila yeye akapandishwa cheo.

 “Huyu aliyepandishwa cheo wakati huo alikuwa Mkuu wa Idara ya Fedha (Mhasibu Mkuu). “Swali ambalo halijapata majibu ni kuwa yawezekanaje meneja mkuu awajibishwe kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya pesa zaSerikali ktk mradi wa matengenezo ya Meli na Mhasibu mkuu ambaye ndiye mshauri wa Meneja Mkuu kwenye masuala ya fedha apandishwe cheo?” anahoji mfanyakazi mwingine.

 Tangu December 2015, pamekuwa na maelezo yasiyokuwa rasmi yaliyokuwa yanawapoza wafanyakazi kuwa Serikali inayaelewa matatizo ya kampuni na inafanyia kazi kero hizo, mara nyingi mameneja wamekuwa wakienda wizarani wakidai kuitwa wakawasilishe serikalini changamoto na mahitaji ya Kampuni.

 Pia inadaiwa kuwa viongozi wengi wamekuwa wanakienda na kukomea makao makuu kwa siku tatu mpaka wiki nzima kujiridhisha na kuchukua taarifa za msingi kwa ajili ya Serikali kuchukua  hatua sahihi katika kutatua matatizo ya kampuni, lakini mpaka sasa hakuna matunda ya safari za mameneja na ugeni kutoka wizarani ambao umekuwa ukitembelea kampuni.

 “Ifahamike kuwa gharama za safari na posho za mameneja na hao viongozi toka wizarani au serikalini zimekuwa zikilipwa na MSCL,” anasema mmoja wa maafisa waandamizi wa kampuni hiyo.

Mpaka sasa Serikali imesimamisha watu katika awamu mbili kama ifuatavyo:

AWAMU YA KWANZA, December 2014:

1. Meneja Mkuu – 01,

2. Meneja Masoko – 01,

3. Mhasibu Mkuu – 01; na

4. Meneja Tawi – 02 ( Mwanza na Kigoma).

AWAMU YA PILI, February 2016:

1. Meneja Mkuu – 01,

2. Meneja Rasilimali Watu – 01,

3. Meneja Ugavi – 01; na

4. Mratibu wa Mradi Maalumu wa Ujenzi wa Meli Mpya – 01.

Hao wote waliosimamishwa bado wanalipwa mishahara, na inatajwa kuwa ni mzigo kwa kampuni ikizingatiwa kuwa nafasi zao zilishakaimishwa watu wengine wanaolipwa mishahara vile vile. “Swali linalozunguka bila majibu ni kwa nini mtu asimamishwe kazi muda mrefu kiasi hicho bila kufikishwa kwenye vyombo husika na sheria ichukue mkondo wake kwa atakayebainika kuwa ana kesi ya kujibu na asiyehusika ama arudishwe kazini au asitaafishwe kwa manufaa ya Umma?” anahoji mtumishi wingine.

 Wafanyakazi hao wanasema Serikali imekuwa ikilipa mishahara ya watumishi wa taasisi za umma zinapokwama kwa sababu zinazoeleweka na zilizo nje ya uwezo wa taasisi  hizo, lakini wao imewaacha. “Mfano wa mashirika ya Serikali yaliyowahi na yanayolipiwa mishahara na Serikali ni ATCL, TRL, TAZARA na RAHACO. Kwa nini suala la mishahara ya wafanyakazi wa MSCL lisichukuliwe na Serikali? Maana ni wazi kuwa Kampuni imefika hapa ilipo sasa kwa kuwa imekuwa inapunguziwa uwezo wa kujiendesha kwa maamuzi yaliyokuwa yanayotolewa na watendaji walio katika ngazi za juu serikalini.

 “Tunaiomba Serikali isikie kilio cha wafanyakazi wa MSCL na ichukue hatua haraka kuinusuru Kampuni ili huduma za usafirishaji majini kwa kutumia vyombo vya Umma irejee na hivyo kupunguza ukali wa maisha kwa wakazi wa maeneo yaliyo katika mwambao wa maziwa makuu.

“MSCL ndiyo Kampuni pekee hapa nchini inayotoa huduma ya kusafirisha maiti bure na hata nauli kwa abiria na viwango vyake kwa usafirishaji wa mizigo ni nafuu sana. Serikali ifanye uchunguzi wa kina ili kubaini watumishi wachache wasio waadilifu walio na dhamana ngazi za juu wanaoipaka matope Serikali na kusababisha wananchi kukosa imani hasa katika nia njema ya Serikali kuhudumia wananchi wake,” anasema mtumishi mwingine.

 JAMHURI limezungumza na Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuliho aliyepangua hoja zote za wafanyakazi hao na kusema dhambi inayowatafuna ni ushiriki wao katika kulihujumu shirika. “Nashanga kwanza hii story, kwa sababu Jumamosi tarehe 18, mwezi huu, nilikuwa nao Mwanza na nilikaa nao tangu saa 9:00 jioni mpaka saa 12:30 jioni na maswali haya yote ninayo… hawa baadhi yao walishiriki kuhujumu shirika na sasa inawarudi,” amesema Katibu Mkuu Chamuliho.

Alisema suala hili analifahamu vyema na kwamba uhalisia Kampuni ya Marine Services Co. LTD (MSCL) haijawahi kumiliki mali zinazotajwa: “MSCL haijawahi kuwa na mali ambayo imehamishwa. Kampuni iliyogawanywa ilikuwa TRC, Tanzania Railway Corporation and Harbors, ndiyo iligawanywa kwenda MSCL, Kwenda TRL, kwenda TPA. Kwa hiyo siyo suala la mali zao.

“Yenyewe iliundwa Kampuni iwe ya uwekezaji ijiendeshe zile mali zingine ziwe kwenye kampuni nyingine na kila kampuni ifanye kazi, independent (kwa uhuru na ijitegemee) na imekuwa ikifanya kazi mpaka walipoanza kuhujumiana huko. Na niliwambia Jumamosi ile kwamba they were part of the problem (walikuwa sehemu ya tatizo),” amesema Chamuliho.

 Anasema shirika lililovunjwa ni jingine na mali ziligawanywa katika mashirika hayo aliyoyataja na mambo yalikuwa yanakwenda vyema hadi walipoanza uendeshaji mbovu wakaharibu.

 Katibu Mkuu amesema hakuna meli hata moja iliyofungiwa na Sumatra, kwani Sumatra inatungia meli zinazotembea na hizo zilizotajwa ni mbovu. Ametaja mfano wa meli ya MV Butiama kuwa injini yake iko Pamba Engineering, kwa ajili ya matengenezo hivyo hakuna uwezekano wa kuifungia.

Anasema meli ya Serengeti, Victoria na meli nyingine ndogo zipo katika matengenezo, ambapo Serikali katika mwaka huu wa fedha imetenga wastani wa Sh bilioni 50.5 kwa ajili ya kuifufua kampuni hiyo ya MSCL.

Dk. Chamuliho amesema katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga Sh bilioni 20 kwa ajili ya ukarabati wa meli ya MV Victoria na ana uhakika itaanza kazi ndani ya mwaka huu wa fedha, Sh bilioni 21 kama malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya, Sh bilioni 5.9 kwa ajili ya ukarabati wa MV Liemba ya Lake Tanganyika na Sh bilioni 3.6 kwa ajili ya ukarabati wa MV Butiama.

 Hoja kwamba Serikali imetelekeza wafanyakazi, Dk. Chamuliho amesema: “Hawa nilikuwa nao juzi, nimewambia. Inabidi ujue anadai nini na anadaiwa nini? Hawajafanya auditing tangu mwaka 1999, hawajawahi kuwasilisha mahesabu yao. Kwa hiyo sasa hivi inabidi mahesabu yafanywe, ijulikane kwa sababu huwezi ukapeleka kwenye Baraza la Mawaziri ukasema nini kinadaiwa bila kuwa na audited paper (hesabu zilizokaguliwa). Kwa hiyo tunafanya huo mchakato sasa hivi tuone ni nini kinaweza kusaidiwa,” amesema.

 Amesema kati ya hujuma walizofanya wafanyakazi hao ni kuendesha meli kutoka Port Bell Uganda hadi Mwanza bila oil na injini ikaunguza baadhi ya vifaa kwa meli ya MV Umoja. Alisema kuwa mchakato huo unafanyika kwa ajili ya kuwawezesha kufufuka waweze kufanya biashara walipe kodi na gawio Serikalini. “Niliwambia hatuwatupi, tutaifufua na mimi niliwambia kwamba imepangiwa mwaka huu wa fedha Sh bilioni 50.5,” amesema.

 Kuhusu tatizo la wafanyakazi wanaofukuzwa kazi na kuendelea kulipwa, amesema tatizo lilitokana na Bodi ya Kampuni hiyo kumaliza muda wake, lakini sasa Bodi imekwishateuliwa na inapitia makosa ya watumishi hao kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, akasema:

 “Baada ya kugundua hizo tuhuma hizo, watu walisimamishwa wakawekwa wengine. Anayetakiwa kuwashughulikia hao, yaani mamlaka yao ya nidhamu ni Bodi. Bodi iliisha muda wake, na hivyo kila kitu kikasimama. Walioingia nao, wakatafuna kama mchwa, ikabidi nao wasimamishwe… wakala kwa speed kubwa kuliko walioondolewa, ikabidi tuwaondowe na kuweka wa muda… niliwaeleza vizuri, ikaonekana kama wameelewa, lakini naona hawakuelewa.

 “Katika hili niliwambia hakuna malaika. Na ninyi mmo, inawezekana na sisi tulikosema, lakini katika hili lazima tufanye audit tujue nani anafanya nini tusije tukakuta tunalipa wafanyazi hewa,” amesema Katibu Mkuu na kuongeza kuwa wafanyakazi hao watapata haki zao baada uhakika kufanyika.

 Hadi sasa wananchi wanakosa fursa ya usafiri wa majini kutokana na meli nyingi kusimamishwa na mara kadhaa Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi kufanya ukarabati lakini haikufanikiwa kufanya hivyo. Hatua ya kutenga Sh bilioni 50, inaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa taifa kujikuta linaondokana na ubovu wa meli na hivyo kurejesha huduma nafuu kwa wananchi.