Watu 38 wameuawa Magharibi mwa jimbo la Darfur nchini Sudan, baada ya wanamgambo wa RSF kutumia ndege isiyokuwa na rubani, kutekeleza shambulio hilo.

Wanamgambo wa RSF wamerusha makombora manne kuwalenga watu kwa mujibu wa wanaharakati, wanaosema mashambulio yameendelea kuongeza katika mji wa El Fasher.

Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo wa RSF wameendelea kudhibiti karibu eneo lote la jimbo la Darfur na kuchukua baadhi ya maeneo Kusini mwa jimbo la Kordofan katika mapambano dhidi ya wanajeshi wa serikali.

Mbali na mauaji hayo ya mwishoni mwa wiki ilitopita, watu wengine tisa walipoteza maisha Ijumaa iliyopita na kuwajeruhi wengine 20 katika mji wa El-Fasher.

Tangu kuanza kwa vita kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF mwezi Aprili mwaka 2023, kuchukua udhibiti wa serkali ya Sudan, maelfu ya watu wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya Milioni 11 wakiwa wakimbizi, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.