Watu watatu wamefariki dunia wakiwemo wanandoa ambao ni askari polisi Mkoa wa Arusha, Noah Semfukwe (30) na Agnes Kiyeyeu (27), katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Tanangozi, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa siku ya Jumanne, Desemba 20, 2022.

Noah na Agnes wamefikwa na mauti katika ajali hiyo ikiwa ni siku nne zimepita tangu walipofunga ndoa, Desemba 17, 2022 jijini Arusha.


Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa, waliofariki katika ajali hiyo ni watatu wakiwemo askari wawili wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Noah Semfukwe (30) aliyekuwa dereva na mkewe, Agnes Kiyeyeu (27).

Mwingine aliyekuwa kwenye gari dogo ni, Enocka Mbata (35), mkazi wa Iringa aliyekuwa kwenye gari hilo ambaye mwili wake umezikwa leo mkoani humo.


Kamanda huyo amesema, ajali hiyo ilitokea saa 3:05 asubuhi wakati gari hilo dogo aina ya Vits kulipiga katika tuta kubwa, ikaenda kwa kasi mbele na kukawa na lori mbeye yake, ikamlazimu kulipita, “ndipo akakutana na basi la Luwinzo uso kwa uso.”

Amesema miili ya askari hao imehifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kesho Alhamisi, itasafirishwa kwenda Makongorosi, Mkoa wa Mbeya kwa maziko