Shirika la Afya Duniani WHO linasema zaidi ya watu 300 wamefariki katika mlipuko wa kipindupindu nchini Sudan

Mlipuko huo unafuatia mvua kubwa na mafuriko yaliotatiza huduma za afya na kuzusha hatari ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama dengue na homa ya uti wa mgongo au meningitis.

Akizungumza katika mkutano na waandishi habari huko Geneva, msemaji wa WHO, Margaret Harris, amesema zaidi ya visa elfu kumi na moja vya ugonjwa wa kipindupindu vimeripotiwa, lakini huenda idadi hiyo ikawa juu zaidi.

“Tunaona ripoti za kipindupindu, surua, malaria, dengue na homa ya uti wa mgongo kutoka majimbo kadhaa. Mpaka sasa tuna visa 11,327 vya kipindupindu vilivyoripotiwa kutoka majimbo 12 na vifo 316.”

Mzozo unaoendelea nchini Sudan kati ya serikali na kikosi maalum cha RSF kimezidi kutatiza huduma za afya na kuifanya hali ya kibinaadamu ambayo tayari ni mbaya kuwa mbaya zaidi. Margaret Harris anasema mfumo wa afya unasambaratika.

“Kuna uhaba wa dawa na vifaa vya matibabu, maafisa wa afya na hata pia fedha. Wahudumu wa afya hawalipwi kwa hivyo wanajitahidi.

Hawalipwi na hawawezi kununua vifaa kwasababu kuna uhaba wa pesa,” ameongeza Margaret.

Please follow and like us:
Pin Share