Wakili wa Serikali katika Ofisi ya Wakili Mfawidhi Kanda ya Moshi, Omari Kibwana, anadaiwa kuwa si raia wa Tanzania kwa kuzaliwa.
Kwa tuhuma hizo, Idara ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro imefungua jalada la uchunguzi ili kubaini ukweli.
Kibwana ambaye amekuwa wakili wa serikali kwa muda mrefu, anatuhumiwa kuwa ni Mkenya kwa kuzaliwa na hajawahi kuukana uraia wa nchi hiyo.
Mkuu wa Uhamiaji Mkoa (RIO) wa Kilimanjaro, Albert Rwelamira, ameliambia JAMHURI kuwa wanamchunguza Kibwana na endapo atabainika kuwa si Mtanzania, atatakiwa ama aombe [arekebishe] au aondoke nchini.
“Suala lake tunalo na tunaendelea nalo. Tunapoletewa tunachunguza na tukiona kuna jambo tunamshauri mwajiri wake, tunamwambia kuwa huyu uliyenaye siyo,” amesema.
Amesema Kibwana ni mtumishi wa umma, kwa hiyo hawawezi kufuta ajira wala kuondolewa nchini hadi ukweli utakapobainika.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Kanda ya Moshi, Abdallah Chuvula, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, badala yake ametaka atafutwe Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Kwa upande wake, Kibwana, amehoji mbinu alizotumia mwandishi kupata taarifa zake lakini akasisitiza kuwa yeye ni Mtanzania halali.
Wakati huo huo, Idara ya Uhamiaji mkoani Kilimanjaro imewafukuza nchini walimu wanne ambao ni raia wa Kenya baada ya kubainika kuwa waliingia nchini na kufanya kazi bila vibali wala hati za kusafiria.
Walimu hao walikamatwa wakiwa wanafundisha katika Shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo Himo, Moshi Vijijini. Pamoja na kutakiwa kuondoka, wametozwa faini ya dola 600 za Marekani kila mmoja.
Uhamiaji imemuonya mmoja wa wakurugenzi wa shule hiyo, Scolastica Matemba (Mama Scolastica) kwa kuajiri raia wa kigeni bila kufuata taratibu. Hata hivyo Matemba amekana shule yake kuajiri walimu wasio raia.
Pamoja na Wakenya, raia wengine wawili wa Uganda wamekamatwa wakiwa hawana vibali vya kufanya kazi nchini.