Mcheza soka maarufu wa zamani Ronaldo De Lima wa Brazil, amepewa majukumu ya kuzindua rasmi fainali za Kombe la Dunia 2018 kwenye mechi ya ufunguzi kati ya wenyeji Urusi dhidi ya Saudi Arabia Alhamisi ya Juni 14.
Kwa mujibu wa FIFA Ronaldo atakuwa na jukumu la kupeleka uwanjani Kombe la Ubingwa wa Dunia ambalo mataifa 32 yaliyofuzu yatakuwa yanaliwania. Ronaldo atatambulisha Kombe hilo tayari kwa kufungua mashindano hayo ambayo yatamalizika Julai 15.
Mbali na Ronaldo shughuli nzima ya burudani kwenye ufunguzi huo itasimamiwa na mwimbaji wa Pop kutoka nchini Uingereza Robbie Williams ambaye ataungana na msanii wa Urusi Aida Garifullina.
Seherehe za ufunguzi wa fainali hizo zitaanza majira ya saa 6:00 mchana kwenye uwanja wa Luzhniki jijini Moscow. Urusi na Tanzania zinaendana kwa saa isipokuwa katika mij kadhaa.
Ronaldo De Lima amechukua Kombe la Dunia mara 2 akiwa na timu yake ya taifa Brazil mwaka 1994 na 2002. Pia nguli huyo allibuka mfungaji bora wa fainali za mwaka 2002 kwa kufunga jumla ya mabao 8.