Na Mwandishi Wetu, JamburiMedia, Dar
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limefanya mageuzi makubwa ambayo yameliwezesha shirika hilo kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 1.3 hadi shilingi bilioni 61.1 sawa na ongezeko la asilimia 4425.
Hayo yamebainishwa leo Agosti 28,2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, CPA Dkt.Venance Mwasse katika kikao kazi kati ya shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, mafanikio hayo yameliwezesha shirika sasa kuanza kutoa gawio serikalini, kwani tangu lianzishwe mwaka 1972 lilikuwa halijawahi kupeleka kitu chochote serikalini.
Dkt.Mwasse amefafanua kuwa, sababu zilizowawezesha kufikia mafanikio hayo ni kwa kubadili fikra,ushirikishwaji, nidhamu, kujiwekea malengo na kuyatekeleza.
“Kwa ujumla, tulifikia mahali ikabidi tubadilike kifikira, kuna mashirika ya umma ambayo yanayotoa huduma na kuna mashirika ya umma ambayo yanatakiwa yajiendesha kibiashara.
“Kwa hiyo tulipoamua kujiendesha kibiashara, tukaamua sasa kwenda kuzitafuta fursa, tulipobonyeza hiyo button tukaona mambo yamekwenda.
“Na mimi kama kiongozi kwa kulitambua hili ni shirika la umma nikaona lazima tuumize vichwa, pamoja na kuongeza morali ya wafanyakazi kwa kuona wanajaliwa na mipango iwe inanyooka.
“Pamoja na kuongeza nidhamu kwenye matumizi ya fedha za umma, na tuchague sehemu sahihi, kwa sababu sehemu za kuweka fedha ni nyingi, hivyo unaangalia penye faida.
“Maendeleo huwa yanapagwa kwa hiyo, mnapopanga mambo, lazima yafanyike, mnapanga pamoja na lazima utekelezaji ufanyike, lakini kama kiongozi lazima ufanye maamuzi ambayo yana manufaa kwa umma, makubwa na yenye mageuzi kama hayo.”
Katika hatua nyingine, Dkt.Mwasse amesema, wanaendelea kungeza uzalishaji wa mkaa mbadala ili kuondoa matumizi ya mkaa unaotokana na miti na matumizi ya kuni.
“Mikakati yetu ni kuendelea kuzalisha kwa wingi ili kuendelea kuwa kimbilio na tumani kwa watumiaji wengi nchini.
Wakatio huo huo, Dkt.Mwasse amebainisha kuwa, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezidi kufanya vizuri katika shughuli za uchorongaji madini nchini.
Amesema, ufanisi wao ndiyo umewawezesha kusaini mkataba mnono wa kuchoronga na mgodi mkubwa na Geita Gold Mine (GGML) uliopo mkoasni Geita.
Mkataba huo ambao una thamani ya bilioni 55.2 na ulitiwa saini Machi 27,2023.
Dkt.Mwasse amesema, mkataba huo ni uthibitisho kuwa watanzania wanaweza kushiriki kikamilifu katika kandarasi zinatokea katika mnyororo wa thamani wa madini nchini.
Pia amesema, wanajivunia kufanya kazi na GGM kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kwa mfululizo na kwa kipindi chote wamekuwa na ushirikiano mzuri.
“Kwa hiyo tutaendelea kuimarisha tasnia ya uchorongaji, mradi ambao sisi ni kinara.”
Pia, STAMICO imejipanga kuwaendeleza na kuwarasimisha kabisa wachimbaji wadogo.
“Tumeweka jicho letu la kipekee hapa, tutaendelea kuwapa mafunzo, na kubwa zaidi tutahakikisha benki ya wachimbaji inaanzishwa ili kuondoa changamoto ya wachimbaji, mpaka sasa hivi hakuna benki ya wachimbaji.
“Kwa hiyo tunaamini pamoja na kuwaunganisha na benki mbalimbali, lakini tunaamini benki hii itakuwa mkombozi kwao.”
Hata hivyo, Dkt.Mwasse amesema, kupitia mikapango na mikakati thabiti ya shirika hilo wanatarajia ifikapo mwaka 2025, shirika liwe linajitegemea.