ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu

Mwanasiasa mkongwe, Baraka Mohamed Shamte, amemtaka Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-  Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, kuacha kauli za upotoshaji.

Moja kati ya kauli anazodai zimetamkwa na Jussa ni madai kwamba CCM haina dhamira njema katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). 

Shamte ameelekeza lawama kwa viongozi wa ACT – Wazalendo, akidai kuwa ni wao ndio wasioheshimu maridhiano na utangamano. 

“Kupatikana kwa umoja na utulivu wa kisiasa, ustawi wa amani na upendo ndiyo malengo yetu. Wao wasiitake CCM kubweteka na kutojipanga kushinda katika Uchaguzi Mkuu au mdogo wa majimboni,” anasema Shamte. 

Anayaita matamshi ya Jussa kuwa na lengo la kuilazimisha dunia ikubali kuwa CCM wanaibembeleza ACT-Wazalendo kuwamo SUK. 

Anasema kila chama kinapaswa kuenzi na kulinda amani, akiongeza kuwa madai ya kutokuwapo misaada kutoka jumuiya za kimataifa hadi chama chake kitakaposhinda, ni vitisho visivyokuwa na tija. 

“Propaganda hizi zinaenezwa kwa nguvu na ACT – Wazalendo kukionyesha chama hicho hakiwezi kushindwa; kwamba ndicho kinachokubalika kuliko vingine vyote hata kama ni CCM ndiyo inayoongoza dola kwa miaka mingi sana.

“Umoja, utulivu na mshikamano wa Wazanzibari hautegemei huruma ya chama fulani. Watu waache kujigamba na kuwapotosha walimwengu. Wajipange kujenga chama chao,” anasema Shamte.  

Anasema chama hicho kimepoteza mwelekeo wa kisiasa na sasa hakina tena uwezo wa kupambana na CCM kwenye uchaguzi huru kupitia masanduku ya kura kutokana na kuendeleza na kuendekeza siasa za mitandaoni. 

Akijibu kauli za Shamte, Jussa anasema mwanasiasa huyo ni kati ya vizingiti vilivyoikwamisha Zanzibar kupiga hatua mbele za kimaendeleo na kwamba hajui anachokisema kwani ni kigogo mwenye mtazamo wa kihafidhina. 

Jusa aanasema asingependa kujibishana na Shamte, kwa kuwa ni mkereketwa ambaye hana nafasi wala mamlaka yoyote ndani ya CCM. 

Kwa upande mwingine, Shamte anasema ACT – Wazalendo wanapwaya kisiasa kutokana na kuondokewa na kiongozi aliyekuwa na mvuto zaidi, Maalim Seif Sharif Hamad. 

“Hawajashurutishwa kwa nguvu kushiriki SUK. Sasa iweje kila wanaposhindwa uchaguzi viongozi wake wanadai kwamba Zanzibar kuna mgogoro? 

“Chama hicho kisimtishie Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi. Hata mwaka 2015 waliposusia matokeo, Rais mstaafu, Dk. Ali Mohamed Shein, alivishirikisha vyama vingine,” anasema.

Shamte ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Zanzibar baada ya uhuru wa mwaka 1963, anasema dunia ina haki ya kuzifuatilia siasa za chama hicho ambacho kimekuwa mashuhuri kwa kuandika barua kwa mabalozi na jumuiya za kimataifa.