Mshambuliaji wa Liverpool, Mtaliano Mario Balotelli, ndiye mchezaji aliyebaguliwa zaidi katika Ligi Kuu ya England, imefahamika.
Taarifa zinasema kwamba mchezaji huyo hupokea ujumbe wa aina mbalimbali katika mitandao ya Twitter, Facebook, Instagram na WhatsApp ambako jumla yake ni 8,000 kwa siku.
Lakini wakati akipokea mjumbe huo, asilimia 50 yake umekuwa ni wa kibaguzi kiasi cha kumfanya nyota huyo wa zamani wa Manchester City, kupuuza.
Takwimu hizo za kushtua zimeripotiwa na mtandao wa Kick it Out zikisema mshambuliaji wa Arsenal, Danny Welbeck, naye hupokea ujumbe wa kibaguzi asilimia kama 20. Hupokea ujumbe wa kumbeza kwa sababu ya rangi yake.
Mshambuliaji mwenza wa Balotelli katika Klabu ya Liverpool, Daniel Sturridge, pia alionekana kulengwa katika mitandao ya kijamii baada ya kupokea ujumbe wa 1,600 asilimia 60 ikiwa ni ujumbe wenye mwelekeo wa kijinsia.
Utafiti huo pia umebaini kuwa Klabu ya Chelsea ndiyo klabu iliyobaguliwa zaidi kwa kupokea ujumbe 20,000 huku Liverpool ikiwa ya pili na ujumbe 19,000, Arsenal ikiwa ya tatu kwa ujumbe 12,000 huku Manchester City na Manchester United zikipokea ujumbe 11,000 kila mmoja.