Aprili 2013, kupitia safu hii, niliandika makala ndefu iliyosema: “Bila kudhibiti NGOs, Loliondo haitatulia”. Makala hiyo ipo kwenye mitandao mbalimbali.
Kuandika masuala ya Loliondo kunahitaji ujasiri. Mosi, lazima mwandishi akubali kutukanwa. Sharti awe tayari kutishiwa maisha kwa sababu maandiko yake yanatishia ulaji wa watu.
Pili, anayetaka kuandika masuala ya Loliondo sharti atie pamba masikioni kwa sababu atarushiwa maneno makali-na hata kuhusishwa na rushwa.
Raia wa Sweden, Susanna Nordlund, nikijibizana naye kwenye barua pepe hivi karibuni, aliandika haya: “I don’t understand why you behave this way. Are you being paid enormous sums or are you just an evil person? I hope someone will investigate you.” Anastajabu kwa nini nimeamua kuwa kama nilivyo! Ana shaka kama msimamo wangu hautokani na kulipwa fedha (rushwa) ili niwe hivyo. Kiu yake ni kuona nachunguzwa!
Maneno haya huyatarajia pindi ninapoamua kuandika masuala yanayoihusu Loliondo. Susanna ni jasusi wa kiuchumi na mmoja wa Wazungu wanaofaidika kwa uendelevu wa migogoro isiyokoma katika Wilaya ya Ngorongoro, na hasa sasa katika vijiji vya Tarafa ya Loliondo.
Hivi sasa ninavyoandika makala hii, Susanna yuko ndani ya Loliondo katika eneo la Posmoro licha ya kuwa ameshapigwa PI mara mbili. Anaingia akitokea Kenya na kurejeshwa huko kwa msaada wa NGOs. Anaichezea Serikali ya Tanzania atakavyo. Upuuzi huu hauwezi kufanywa na Mwafrika nchini Sweden au kwingineko Ulaya. Hii ni dharau kubwa. Serikali inapaswa kuonesha kuwa ipo na inafanya kazi. Wanaomwezesha kutenda dharau hii wanapaswa kushughulikiwa kisheria maana ni aibu na hatari kwa usalama wa nchi yetu.
Susanna ana marafiki zake wa Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Pastoral Women Council (PWC). Shirika hili linaongozwa na Maanda Ngoitiko. Juzi tu, viongozi wawili wa Loliondo kwa pamoja waliandika makala wakieleza ushiriki wa PWC na Susanna katika kuifanya Loliondo isitawalike. PWC wameleta kusudio la kulishitaki Gazeti la JAMHURI na waandishi wa makala hiyo- William Mosongo Alais – Diwani wa Kata ya Oloipiri na Gabriel Kamomon Olle Killel – Mkurugenzi wa Shirika la KIDUPO Integrated Development Peoples’ Organization.
PWC wanajaribu kuonesha kuwa hawana uhusiano na Susanna. Wanataka ijulikane kuwa wana msaada mkubwa kwa wana Ngorongoro! Hii ni mada nyingine inayojitegemea, lakini niseme tu kuwa huu ndiyo wakati mzuri wa kuijua PWC na wafadhili wake. Mpango Mkakati wao wa mwaka 2012-2016 umeeleza kila jambo. Makala zijazo nitawaeleza wasomaji.
Tumekuwa sehemu ya waliokomalia Loliondo kwa kuwa tunaamini tuna wajibu wa kufanya lililo jema kwa nchi yetu.
Tuna wajibu wa kuwasema mamluki walio nje na ndani ya nchi yetu ili Serikali iweze kuwatambua na kuchukua hatua zinazostahili kwa lengo la kuulinda Uhuru wetu. Muda wa kuyumbishwa na raia wa kigeni na mawakala wao umeshakwisha.
Ngorongoro kuna NGOs zaidi ya 30! Akili ya kawaida tu inaweza kumtuma mtu kujiuliza sababu ya kuwapo utitiri huu wote. Suala la utetezi wanaohubiri ni kiini macho. Kinachofanywa na mashirika haya ni kuitumia migogoro hii kama chanzo maridhawa cha mapato. Wanajua uhai wao utawezeshwa tu na uendelevu wa migogoro na ndiyo maana kunafanywa kila linalowezekana kuhakikisha kuwa Loliondo haitulii. Wanajua ikitulia, hakuna fedha zitakazoingia kwenye akaunti zao.
NGOs hizi zinakusanya mabilioni ya shilingi kutoka kila pembe ya dunia, lakini hakuna lolote kubwa la maana ambalo fedha hizo zimetumika kuwasaidia watoto maskini wanaokosa elimu, huduma za afya, maji safi na salama, na kadhalika. Watoto wa wenye NGOs hizi wanasoma International Schools- zilizoko Tanzania, Kenya, Ulaya na kwingineko duniani. Wale watoto wa makabwela wameendelea kupigwa picha na kutumiwa kama chambo cha kuombea fedha k.utoka kwa wafadhili! Ukichunguza zaidi utabaini kuwa Wamasai waliosoma hawataki wenzao wasome! Wanataka waendelee kuwa duni, na uduni huo wautumie kama chanzo cha mapato! Huo ndiyo ukweli
Dunia ya leo bado kuna binadamu wanawatumia binadamu wenzao kama chanzo cha mapato! Haya ndiyo ya Loliondo.
Kuna NGOs zinazowaongopea wafadhili kwa kutaja miradi iliyotekelezwa na Serikali kuwa imetekelezwa kwa fedha za wafadhili. Mfano mzuri wa NGOs hizo ni PWC. Hili lipo kwenye maandishi yao wenyewe! Haya tutayasema hata kama kwa kufanya hivyo kutahatarisha hatima yetu.
Miongoni mwa watu hatari kwenye mgogoro wa Loliondo ni Susanna. Huyu anafanya kila analoweza kuingia Loliondo kuhamasisha vurugu. Anasaidiwa na watu wanaojinasibu kuwa ni Watanzania, ilhali ukweli ukiwa kwamba ni mamluki.
Raia huyu wa kigeni akijua kuna fedha atazipata kwa kuhamasisha vurugu, aliingia nchini mara ya kwanza mwaka 2010 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Alipofika Arusha, aliishi katika hoteli ya Flamingo kisha akaenda Wasso, Loliondo ambako huko alizuru vijiji vya Sukenya na Soitsambu.
Kwa maelezo yake mwenyewe, alikwenda Loliondo si kwa lengo la kutalii, bali kufuatilia malalamiko ya wanakijiji wa Sukenya dhidi ya mwekezaji- Thompson Safaris. Miongoni mwa wenyeji wake ni PWC. Akataka eti kujua kama yalikuwa ya kweli au la! Anasema jamii ilikuwa ikilalamikia Thompson kuwa imechukua ardhi yote ya kijiji na kuwapiga wananchi; tuhuma ambazo zilikuwa za kupikwa ili kuijaza hasira jamii ya kimataifa-na mwishowe iichukie Serikali halali ya Tanzania.
Kwa kufanya hivyo akawa amekiuka masharti ya visa yake ya utalii ambayo alipewa wakati anaingia nchini Januari 21, 2010.
Aliporejea kwao aliandika makala za uchochezi na kuwaonya watalii wasitembelee Loliondo hadi mwekezaji Thompon Safaris aondoke Tanzania!
Susanna ni mwalimu wa lugha ya Kispaniola lakini hafundishi, badala yake maisha yake yote kwa sasa yanatokana na kuchochea migogoro Loliondo. Anaishi kwa kuandika makala zenye kuichafua Tanzania na kupata ufadhili wa mamilioni ya fedha. Yeye mwenyewe kupitia barua yake ya Aprili 3, mwaka huu kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anasema: “Sioni hatma yangu bila kutembelea Tanzania…”
Alimwandikia barua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wa wakati huo, Charles Kitwanga, akitaka aondolewe PI ili aweze kuingia nchini. Nakala ya barua hiyo aliipeleka Ubalozi wa Sweden jijini Dar es Salaam, Ubalozi wa Tanzania ulioko Stockholm, Sweden; na kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Wallstrom.
Mkuu wa Wilaya ya wakati huo, Elias Wawalali aliongoza shughuli ya kumkamata Februari, 2010. Akapelekwa Uhamiaji na akakutwa na hatia ya kuendesha mikutano kwa wananchi bila kibali. Apigwa faini ya dola 400 za Marekani. Akapewa hati ya kufukuzwa nchini (PI Na. 0039131) iliyotolewa Februari 12, 2010 Arusha. Hati yake ya kusafiria yenye namba 12011727 aliyoipata Sweden Februari 8, 2001 ikagongwa muhuri kuonesha kuwa hatakiwi kuingia Tanzania.
Aliporejea Sweden akafungua blog ya “view from the Termite Mound”. Huko akajaza makala za uchochezi zinazoendelea kuitafuna Tanzania.
Pamoja na kupewa PI mwaka 2010, Susanna alibadili hati ya kusafiria na kurejea nchini Septemba 2011 kupitia Namanga akitumia hati yenye namba 825 623 97 iliyotolewa Sweden.
Alipitia Namanga akitokea Kenya ambako NGOs nyingi za Ngorongoro, ama zinamilikiwa, au zina ushirikiano mkubwa na Wakenya.
Hapo Namanga alipewa viza ya utalii. Aliingia kwa kutumia hati yenye namba 82562397 iliyotolewa Sweden. Akafikia katika hoteli ya Abba iliyoko Arusha kisha akaenda loliondo na kuzuru vijiji vya Ololosokwan, Mondorosi, Sukenya, Soitsambu na Kirtalo. Kumbukumbu hizi zipo!
Akazungumza na wanavijiji na baada ya hapo akaandika makala nyingi za uchochezi zilizolenga kuwafanya wananchi waichukie Serikali yao halali.
Alirejea nchini kwa mara ya pili Juni, 2013 kwa kupitia hapo hapo Namanga na kupewa viza ya utalii. Akafikia katika hoteli ile ile ya Abba jijini Arusha kabla ya kuzuru vijiji vya Loliondo vya Ololosokwan, Mondorosi, Sukenya na Kirtalo kwa lengo lile lile la kueneza chuki dhidi ya wawekezaji na Serikali.
Akadandia uamuzi wa Serikali wa kutwaa eneo la kilometa 1,500 za mraba kwa ajili ya ushoroba wa wanyamapori. Akasema wananchi walikuwa wakipokwa ardhi yao. Akashiriki kuhakikishia wananchi wanaasi na kutishia kujitoa CCM. Kwa woga wa viongozi wa wakati huo, Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ikasalimu amri. Athari za uamuzi huo zinaonekana wazi leo. Loliondo inakufa.
Aliporejea kwao akaandika makala nyingi za uchochezi akimshutumu Waziri wa Maliasili na Utalii na viongozi wa Serikali ya Tanzania.
Juni 17, 2015 akiwa na PI, aliingia nchini kupitia kwneye upenyo wake wa Namanga na kupatiwa viza ya utalii! Wawezeshaji wa mpango huu ni NGOs zinazomuunga mkono kwenye uchochezi huu. Alifikia Monjis Guest House, Arusha ambako alikaa kwa siku tatu kisha akaenda Loliondo Juni 20.
Kule Loliondo alifikia Oloip Lodge iliyopo Wasso. Maudhui ya safari hii alikuwa azungumze na wanavijiji. Alikamatwa na Uhamiaji, Polisi, Usalama wa Taifa Wilaya ya Loliondo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya wa wakati huo, Hasshim Mgandilwa. Alikamatwa Juni 23, 2015 akiwa anakula na kunywa katika baa ya Kwa Honest majira ya saa 2 usiku.
Alipokaguliwa alikutwa ameandaa maswali kadhaa ya ushushushu ya kuwauliza wanavijiji wa Kitralo, Mondorosi, Sukenya na Soitsambu.
Aliwekwa rumande na siku iliyofuata alipelekwa Ofisi ya Uhamiaji, Loliondo kwa mahojiano. Akasafirishwa kwenda katika Ofisi za Uhamiaji Mkoa jijini Arusha na huko akapewa PI nyingine na kufukuzwa nchini.
Kwa kipindi chote ambacho amekuwa akiingia nchini, alikuwa akikiuka Sheria za Uhamiaji kwa kuingia kama mtaalii, lakini hakuwahi kufanya utalii wowote zaidi ya kufanya mikutano ya siri na wanavijiji ili waichukie Serikali yao halali pamoja na wawekezaji ambao kiuhalisia ni msaada mkubwa kwa Wilaya ya Ngorongoro na Taifa.
Taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro inaonesha kuwa mwekezaji kama OBC amechimba visima 50 vya maji katika kata zote za Tarafa ya Loliondo. Kila kisima kimoja kimegharimu shilingi zaidi ya milioni 50.
OBC wamejenga shule nyingi nzuri, hospitali ya kisasa, madaraja na huduma nyingine nyingi za kijamii.
Thompson amejenga shule, zahanati na kutoka michango katika vijiji vingi vinavyozunguka eneo analofanyia kazi. Hakuna NGO iliyofanya haya licha ya kupokea mabilioni ya shilingi kila mwaka.
Susanna na wenzake wanajua hawafanyi lolote la maana zaidi ya kujinufaisha wao tu. Pale anapobaini utulivu ukianza kurejea Loliondo, amehakikisha anahamasisha mifugo ichungwe katika maeneo ya wawekezaji na hata kuvushwa hadi ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, akisema ni haki yao ya asili kuyatumia maeneo hayo! Leo Serengeti inakufa. Mifugo, maelfu kwa maelfu kutoka Kenya inanenepeshwa Loliondo na hifadhini Serengeti.
Amefanya kila linalowezekana Ngorongoro isitawalike kwa kuhakikisha wananchi wanazisikiliza na kuzitii zaidi NGOs badala ya Serikali. Wananchi wanahamasishwa wasiwe tayari kutii maelekezo yoyote ya kisheria. Anatumia tovuti yake kuendeleza chuki na kuupotosha ulimwengu juu ya hali halisi ya Loliondo.
Loliondo inahitaji kutazamwa kwa jicho la pekee. Waziri Mkuu Kasssim Majaliwa na wasaidizi wake wakae wakijua Loliondo kuna NGOs zinazoua uhifadhi. Wajue Loliondo sasa ni kama serikali ndani ya Serikali. Uhifadhi umekufa kwa sababu NGOs na kina Susanna wanahamasisha kilimo kila mahali. Wanyamapori wamekimbia. Hifadhi ya Serengeti imeshavamiwa na wafugaji hadi kilometa 20 ndani.
Susanna hajakoma. Anaendelea kufanya kila mbinu kuingia Loliondo kuendeleza uchochezi. Wenyeji wake wanajulikana. Wanatamba.
Ustawi wa Loliondo hauwezi kuletwa na NGOs ambazo ni mawakala wa Wazungu wanaokusanya fedha kutoka kwa wafadhili ili wajinufaishe wao wenyewe. Na kama kuna NGOs inadhani imefanya jambo la maana kuwasaidia wana Loliondo kuondokana na umaskini, na isimame inisute! Haipo.
Waziri Mkuu usiiweke kando Loliondo ambayo imevamiwa na raia wengi mno wa kigeni. Nenda ukajionee mwenyewe. Loliondo inakufa. Ngorongoro inakufa. Uhifadhi unatoweka. Haya tunayasema ili historia isituweke kwenye kundi la wasaliti waliokaa wakati nchi na uhifadhi vikiteketea. Hatua za kuikoa Loliondo na Ngorongoro zianzie kwenye udhibiti wa NGOs na mawakala wao wa uchochezi aina ya Susanna ambao wanasema bila soni kwamba “hawaoni hatima yao bila kufika Loliondo”.