Mgogoro wa masilahi katika Pori Tengefu la Loliondo (LGCA) unafukuta upya baada ya Watanzania takriban 20 kutarajiwa kusafiri kwenda nchini Uingereza wiki hii kuomba fedha za kuendeshea mapambano dhidi ya serikali.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa harambee ya kukusanya fedha hizo imeandaliwa na asasi ya The Oakland Institute ya nchini Marekani.
Fedha zinazotarajiwa kukusanywa, pamoja na mambo mengine, zinalenga kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) wilayani Ngorongoro na mkoani Arusha kuendesha harakati zao dhidi ya mpango wa serikali wa kutenga kilometa za mraba 1,500 kutoka LGCA kwa ajili ya uhifadhi.
Pamoja na viongozi wa NGOs hizo ambazo tuna majina yake, wengine kwenye msafara huo ni baadhi ya viongozi wa vijiji, akiwamo mmoja mwandamizi kutoka Kijiji cha Ololosokwan.
Tayari NGOs hizo zimeanza kuhamasisha wananchi kurejea kwenye maeneo ambayo waliondoka kupisha uhifadhi. Wanahamasishwa kurejea baada ya uamuzi wa Mahakama ya Afrika Mashariki kutaka wasiondolewe hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa. Miongoni mwa wanaorejea kwa kasi eneo hilo wanatoka Kenya na wanaendesha kilimo na kuua uhifadhi.
Wakati hayo yakiendelea, uchunguzi umebaini kuwa NGO moja inayojihusisha na masuala ya utetezi wa wanawake imepokea fedha nyingi kutoka kwa wachochezi wa migogoro hiyo, akiwamo raia wa Sweden, Susanna Nordlund, aliyefukuzwa nchini kwa PI. Fedha za NGO hiyo zinazokisiwa kuwa Sh. bilioni kadhaa, sasa zinatumiwa katika harakati. Akaunti zake ziko nchini Kenya.
Asasi ya Oakland, kwa siku za karibuni imekuwa kinara kwenye migogoro katika Pori Tengefu la Loliondo na sasa inaendesha kampeni ya kile inachokiita uporaji wa ardhi ya Wamasai unaofanywa na Serikali ya Tanzania.
Hata hivyo mapambano yake sasa yanaelekezwa zaidi kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), lengo likiwa kuchochea wananchi waasi, mpango wa serikali unaozuia ongezeko la shughuli za kibadamu na upelekaji wa mifugo katika kreta.
Wanaotajwa kuwa ndio waandaaji wa ripoti hiyo ni raia wa kigeni, Anuradha Mittal na Elizabeth Fraser; ambao wameshirikiana na Watanzania wanaofichwa majina kwa madai ya kulinda usalama wao.
Wiki kadhaa zilizopita JAMHURI liliandika juu ya kuwapo mpango wa taarifa ya Kiswahili ya Oakland Institute inayolenga kuichafua Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Taarifa hiyo iliyokuwa imeandaliwa kwa Kiingereza, hatimaye ilipelekwa kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa ajili ya kutafsiriwa na kuandikwa kwa ufasaha na wataalamu wa lugha. JAMHURI limepata nakala yake yenye kichwa cha habari: “Kuipoteza Serengeti”, ingawa maudhui yaliyomo mengi yanailenga Ngorongoro.
Chimbuko la ripoti ya Oakland ni harakati za NGOs za Loliondo kushirikiana na wahisani kutoka Ulaya na Marekani ili kutimiza njozi za taasisi hizi za kujipatia pesa kwa kutumia dhana ya utetezi.
Jina la ripoti yao limetengenezwa kiufundi ili kusadifu yaliyomo, lakini haliendani kabisa na mada husika. Wanataka kuaminisha ulimwengu kuwa Serengeti, Ngorongoro na uhifadhi kwa ujumla ndiyo chanzo cha matatizo ya jamii ya Kimaasai inayoishi Loliondo.
Sababu za kuandaa ripoti ya Oakland ni kuvuruga uamuzi wa serikali juu ya Loliondo na Ngorongoro kwa jumla. Mambo yanayolengwa ni kuvunga kwa kushawishi wananchi na wadau wa maendeleo ndani ya NCA kupinga mchakato mpya wa matumizi bora ya ardhi, kushawishi wananchi kuwa uamuzi wa serikali juu ya Loliondo unalenga kumlinda mwekezaji (OBC) na si masilahi mapana ya serikali na jamii ya Loliondo.
Ripori ya Oakland inahamasisha kuhamasisha uanzishwaji wa Eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA), jambo ambalo wamewahusisha na kupata baraka za Mbunge wa Ngorongoro, William ole Nasha; na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo. Lengo ni kuhakikisha inaanzishwa WMA na ikiwezekana iwe chini ya mwekezaji, Kampuni ya Afrika Kusini ya And Beyond ambayo ina ushirikiano wa karibu na Nasha na Gambo.
Wahifadhi wanapinga uanzishwaji wa WMA wakisema umuhimu wa Loliondo unapaswa kuwa chini ya uangalizi wa dola, na wananchi washirikishwe kama wadau. Inapandekezwa eneo la kilometa za mraba 1,500 litakalotengwa liwe chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwa kutungiwa sheria maalumu itakayoruhusu pamoja na mambo mengine, uwindaji wa kitalii.
Loliondo inaongoza kwa kuwa na NGOs nyingi ambazo zinategemea pesa kutoka nje ya nchi ili kuendesha maisha yao ya kila siku. Ili kuomba pesa lazima zionyeshe kuna tatizo la kijamii.
NGOs hizo zina ushirikiano wa karibu mno. Kwa mfano, Mkurugenzi wa U-CRT ni mume wa Maanda Ngoitoko ambaye yeye Maanda ni Mkurugenzi wa PWC. Mkurugenzi wa PINGOs ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya U-CRT.
Maanda wa PWC, Makko Sinandei wa UCRT, Cara Scott, Samantha, Fred Nelson, Jese Davie wa Maliasili Initiative na Jack Vell; wote ni wadau kwenye ripoti ya Oakland. Taasisi nyingine zilizo nyuma ya migogoro ya Loliondo ni Africa Initiative (AI) na Minority Rights Group (MRG).
Serikali bado inaendelea na kigugumizi cha kupeleka muswada bungeni wenye kulenga kupitishwa kwa sheria ya kulinda eneo la kilometa za mraba 1,500. Hali hiyo inatajwa kuwa ndiyo chanzo cha kuendelea kuwapo kwa chokochoko kutoka kwa NGOs na wafadhili.