Utafiti nilioufanya kwa takribani miaka miwili kuanzia Aprili 2013 hadi sasa juu ya hali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), nimebaini mambo mengi, lakini kwa makala ya leo nitagusia tu aina ya kiongozi atakayefaa kukiongoza baada muhula wa Rais Jakaya Kikwete kwisha baadaye mwaka huu.
Jambo la kwanza nililobaini ni kwamba ni ukweli usiofichika kuwa chama hicho bado kina nguvu nyingi hasa kwenye vitongoji na vijijini. Yapo maeneo kule vijijini ambako wakazi wake bado wanakitambua kama chama cha Nyerere. Jina la Nyerere linatosheleza mtu kuipigia kura CCM.
Jambo la pili ni kwamba chama hicho kina idadi kubwa ya wanachama wa uhakika wanaotambulika nchini kote kitakwimu. Kina uwezo mkubwa kumtofautisha mwanachama halali na mamluki. Hivyo, kina uwezo wa kuwajua wapiga kura wake hata kabla kura hazijaanza kupigwa.
Jambo la tatu ni kwamba viongozi wa ngazi za chini kuanzia matawi hadi wilaya, wanachapa kazi kwa nguvu zao zote. Wana uwezo mkubwa kutafsiri Katiba ya chama chao kivitendo. Hata ikitokea kutoa adhabu kwa mwanachama, adhabu hiyo itatekelezwa kwa mujibu wa Katiba inavyoelekeza.
Hata hivyo, nguvu za watendaji hawa wa chini zinadhoofishwa na watendaji wa juu kuanzia ngazi ya wilaya hadi Taifa. Tofauti na ilivyo kiutendaji ngazi za chini, taarifa ngazi za juu zikiteremka chini, zinafikishwa katika mfumo wa kuagiza au amri na kwa utii bila shuruti.
Viongozi wa ngazi za juu ikitokea wameshuka chini, basi ujue kuna agizo au amri ambayo inatakiwa kutekelezwa. Bila kutafuna maneno, lipo ombwe kubwa kati ya viongozi wa chini na viongozi wa juu.
Jambo la nne, chama hicho kimesahau kabisa kusimamia na kutetea malengo yaliyoasisiwa na waasisi wa chama. Hali halisi ya CCM ya sasa ni kwamba imepoteza sifa za msingi. Ni vigumu kwa kiongozi yeyote wa CCM katika karne hii kuweza kusimama hadharani na kujipambanua pasipo kutia shaka kuwa ni muumini wa malengo yaliyoasisiwa na waasisi.
Kwa mfano; turejee katika baadhi tu ya malengo ya CCM kama yalivyoainishwa kwenye Katiba toleo la mwaka 2012, sehemu ya kwanza inayohusu imani na madhumuni ya chama.
Katika sehemu hiyo ya kwanza kifungu kidogo cha 5 kinasema; Kwa hiyo malengo na madhumuni ya CCM yatakuwa yafuatayo; fungu (3) – kuhimiza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea kwa mujibu wa Azimio la Arusha.
Sambamba na hilo, fungu (4) kusimamia utekelezaji wa siasa ya CCM pamoja na kuendeleza fikra za viongozi waasisi wa vyama vya TANU na ASP, kama zilivyofafanuliwa katika maandiko mbalimbali ya vyama hivyo.
Aidha, ahadi ya mwanachama kama zilivyofafanuliwa kwenye Katiba inasema rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa; pili cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu. Ahadi nyingine inaweka bayana kwamba nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko.
Haya ni baadhi tu ya malengo ya wanachama wa CCM kama nilivyoyadurusu kutoka kwenye Katiba toleo la 2012. Swali ambalo jamii ingependa kulijua ni kwamba; je, sera ya ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea kwa mujibu wa Azimio la Arusha bado ipo hai? Je, kiongozi gani anaweza kujinasibu kuwa bado ni muumini wa malengo ya chama hicho?
Turejee nyuma ambako niliahidi kutoa taarifa ya utafiti wangu juu ya aina ya kiongozi ambaye CCM itabidi wampate kwa nyakati za sasa endapo wanataka kuvuka Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Utafiti huo umebaini kuwa chama hicho kinabidi kimpate kiongozi wa aina yake Edward Lowassa kwa hapa nchini, na wa aina yake Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, kwa nje ya nchi.
Nimewataja viongozi hao wawili kwa sababu; kwanza, wote wanafanana kifikra, kimuono na kimatendo. Pili, ni watu wenye msimamo mkali; tatu, si wanafiki na nne ni jasiri katika kusimamia kile wanachokifikiria kifanyike.
Nianze na Rais Obasanjo. Historia ya Obasanjo ni ndefu ambayo nakiri sitaweza kuielezea kwa undani kutokana na udogo wa nafasi. Ila tu naweza kumsemea kuwa ni mmoja wa wanaharakati waliosaidia harakati za ukombozi katika Bara hili la Afrika.
Katika uchaguzi uliomalizika nchini Nigeria, Machi 29, mwaka huu, Rais huyo wa zamani aliweka historia iliyotukuka ya kuwa kiongozi (Rais) wa kwanza barani Afrika kujitokeza hadharani kukemea maovu ya chama chake (tawala), hatimaye kuichana chana kadi ya uanachama baada ya kuzuka sintofahamu kati yake na mwenyekiti wa chama hicho.
Huu ni ujasiri wa kipekee. Hakuwa mnafiki kama tunavyowashuhudia baadhi ya viongozi wa CCM, wakiimba nyimbo za kuenzi malengo ya waasisi wa chama hicho nyakati za mchana na kujipambanua kama ndiyo CCM damu, lakini ikifika usiku wanaking’ong’a chama.
Kwa msingi huo, kiongozi pekee anayefanana na Rais huyo mstaafu wa Nigeria (Obasanjo) na ambaye utafiti wangu umebaini angefaa kuiongoza CCM baada ya muhula wa Rais Kikwete kwisha ni Lowassa.
Bila kumung’unya maneno, hivi karibuni baada ya kuona amechoshwa na unafiki unaofanywa na viongozi ndani ya chama hicho, aliibuka na kusema kwamba yeye hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono. Akiwa na maana kwamba wanachama wapewe haki kuamua mtu wanayemtaka.
Katika kipindi chake akiwa Waziri Mkuu, ndiye aliyeamua kusimamia ujenzi wa shule za sekondari (almaaruf sekondari za kata) kote nchini. Leo hii tunashuhudia hata watoto wa wakulima nao wakifaulu kuingia sekondari.
Ni yeye huyu (Lowassa) aliyesimamia maridhiano kati ya nchi kutoka Maziwa Makuu na Misri juu ya kufaidi maji kutoka Ziwa Victoria. Ni kipindi chake tuliposhuhudia mapigano kati ya wakulima na wafugaji yakimalizwa kibusara.
Ujasiri wake huo wa kusimamia mambo magumu bila woga ndiyo ulioigwa ambako ujenzi wa maabara shuleni kote nchini umefanikiwa kwa staili hiyo. Lowassa ni kiongozi ambaye akiamua kusimamia kitu, anakisimamia kikweli kweli na kuhakikisha kinakamilika kwa muda uliopangwa. Heri tumsafishie njia ya matumaini.
Niseme tu kwamba endapo CCM inataka ipate ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, basi hawana budi kumpitisha Lowassa. Utafiti wangu umebaini zaidi kuwa yeye ndiye mtu anayeuzika kirahisi kuliko wengine wote kwa hivi sasa nchini.
Binadamu hakosi kasoro maana si malaika. Ukichukua uwezo wa kiuongozi wa Lowassa, unaona kabisa unazidi dosari ndogo ndogo zinazotumiwa na wapinzani wake kumsema. Kwangu mimi naona kabisa Lowassa ndiye anayefaa.
Mwandishi wa makala hii, John Kibasso, aliwahi kuwa Mbunge wa Temeke (CCM). Kwa sasa ni mwanachama mtiifu wa CCM anayeishi Dar es Salaam. Anapatikana kupitia simu 0713-399004/0767 399004
email: [email protected].