Mtetezi wa uhifadhi katika Pori Tengefu la Loliondo, Gabriel ole Killel, amefungwa gerezani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni chuki kutoka kwa viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambao amekuwa akiwapinga.
Killel ambaye ni Mkurugenzi wa NGO ya KIDUPO, amefungwa gerezani katika kesi mbili tofauti, kati ya tatu zilizofunguliwa dhidi yake.
Akiwa amehukumiwa kesi ya kwanza kutumikia jela miezi sita, amejikuta akihukumiwa tena miaka minne jela kwa kosa jingine ambalo baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI wamesema ni chuki binafsi.
Killel, kwa muda mrefu amekuwa mstari wa mbele kutetea uhifadhi Loliondo, akizipinga NGOs zinazoendesha uchochezi na kupinga mipango ya Serikali katika eneo hilo.
Kesi ya kwanza yenye namba 26/2017 ilifunguliwa na Tina Timan, katika Mahakama ya Mwanzo Ngorongoro; kesi ya pili alihukumiwa na hakimu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuidharau Mahakama; na kesi ya tatu imefunguliwa na familia yake. Kesi hiyo ya tatu ilifunguliwa na mkewe, Elizabeth Emanuel, na kupewa Na. 852/2017. Ilifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Arusha.
“Kesi hii ilifunguliwa Arusha ili kumfanya Gabriel ashindwe kuhudhuria kesi za Lolindo,” kimesema chanzo chetu.
Mambo yalivyokuwa

Akiwa katika Mahakama ya Mwanzo Loliondo, Killel alijikuta akihukumiwa kifungo cha miezi sita jela kwa shauri Na. 38/2017. Hakimu Gasper Malisa ndiye aliyetoa hukumu hiyo.
Juni 24, mwaka jana kulitokea sintofahamu kati ya Killel na Tina (mke wa mbunge wa zamani wa Ngorongoro). Hii ilikuwa ni baada ya Tina kusikika akipiga kelele katika eneo la ofisi za KIDUPO.
“Mama huyu alidai amepigwa na Killel. Baada ya muda mfupi sana, polisi walifika mahala pale na kumkamata na kumweka rumande katika Kituo cha Polisi Wasso. Baadaye kidogo OCD alifika kituoni hapo, na baada ya mahojiano marefu aliamuru Killel apewe dhamana.
“Lakini viongozi aliokuwa na Tina wakitaka asiachiwe hadi Jumatatu (alikamatwa Ijumaa). Wakati huo Tina alipelekwa hospitali kwa daktari ambaye alishapangwa kwa ajili ya tukio la siku hiyo,” kimesema chanzo chetu.

Je, kweli Killel alimpiga Tina?
Kumekuwapo maelezo kwamba kwa siku mingi kuwa Timan na mkewe (Tina) wamekuwa wakitafuta namna ya kumvuruga Killel na wafadhili wake kutoka Norway ambao amekuwa nao kwa miaka zaidi ya 12.
“Nia kubwa ni kumdhoofisha kutokana na kusema kwake ukweli juu ya madhambi yanayotendeka Loliondo yakiongozwa na wawili hao.
“Basi, siku hiyo hiyo ya Juni 24, 2017 wafadhili wa Shirika la KIDUPO walikuwa wamekuja Loliondo kisiri, kufanya mikutano na jamii ya Kimaasai ambayo hapo awali walinyimwa kibali na uongozi wa mkoa (walirudishwa mara mbili kwa miaka miwili mfululizo kwa shutuma za kuchochea mgogoro wa ardhi Loliondo),” kimesema chanzo chetu.

Uongozi wa Kijiji cha Lopolun ambako ndipo KIDUPO ilikojenga shule ya msingi kwa kutumia wafadhili hao, ukasema kwamba lengo ni kumkamata Killel na kumfungia ndani hadi mikutano yote ya wafadhili itakapoisha.
“Jioni hiyo, Mama Sara (mfadhili) na Wazungu wenzake walikuwa wamefichwa baa ya Oloip inayomilikiwa na Tina na Timan.
“Ili mikakati itimie, yafuatayo yalifanyika; mosi, Tina alipangwa kwenda jioni hiyo ofisini kwa Killel kwa lengo la kumkejeli ili afanye fujo yoyote itakayosaidia kumfanya akamatwe.
“Pili, askari polisi waliandaliwa na kumfuata Tina kwa nyuma ili atakapopiga kelele, basi polisi wawe tayari kumkamata.
“Tatu, viongozi wa Kijiji cha Lopolun waliandaliwa ili wawepo Kituo cha Polisi wakati wa tukio.
“Nne, daktari mmoja wa Hospitali ya Wasso mwenye uhusiano wa karibu sana na Tina, alitayarishwa kwa ajili ya kutoa PMT3 pale mama huyu atakapofikishwa hospitalini,” kimesema chanzo chetu.
Akafunguliwa mashitaka ya kutoa lugha ya matusi, kinyume cha kifungu cha 89 (1)(a) cha Kanuni ya Adhabu [R.E.2002] kwamba alimtusi Tina Timan; kudhuru mwili kinyume cha kifungu 241 cha Kanuni ya Adhabu (R.E.2002); na kutishia kinyume cha kifungu cha 89 (2 (a) cha Kanuni ya Adhabu.

“Wakati hili shauri likiendelea mahakamani, na kuonekana kwamba halina uzito mkubwa dhidi yake, ndipo uchochezi ukazidi kuenezwa na wabaya wake wakishirikiana na NGOs zao mpaka ngazi ya familia yake (Killel).
“Watoto na mama yake wakafungua kesi nyingine mahakamani kwa lengo la kumkana Killel kwamba si mzazi wao!
“Lengo hapa, ni kuongeza uzito wa kesi pamoja na kumweka bize ili apoteze mwelekeo kwenye masuala yanayohusu mgogoro wa ardhi Loliondo.
“Mei 22, 2017 Gabriel akapata samansi ya kuhudhuria kesi iliyofunguliwa na familia yake. Kesho yake katika hali isiyo ya kawaida, akahukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa alilodai hakimu kwamba kaidharua Mahakama.
“Kesi hii ilifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Loliondo baada ya walalamikaji kutoa maelezo yao ndipo mshitakiwa alipotakiwa kutoa maelezo yake ya utetezi siku inayofuata.
“Akiwa mahakamani, alimwomba hakimu kuwa suala hilo lilikuwa nzito na hivyo akaomba aweke wakili na kesi ipande kwenda Mahakama ya Wilaya.

“Katika hali isiyo ya kawaida, siku hiyo hiyo hakimu alimlazimisha kutoa utetezi wake. Killel alisisitiza kuweka wakili, ndipo akahukumiwa kwenda jela miezi sita hapo kwa papo. Hakimu alidai ameidharau Mahakama!
“Je, ile haki ya kusilizwa iko wapi? Na je, kosa hili halina faini? Je, ni kwa mtiririko wa maelezo yapi yaliyosababisha kumfunga Killel?”Kimehoji chanzo chetu.
Kutokana na hukumu hiyo, ile kesi ya Tina ikapata nguvu wakati Killel akiwa gerezani akitumikia kifungo cha miezi sita.
“Wakati akiendelea kutumikia kifungo hiki (miezi sita) ndipo hukumu nyingine ya kesi ya Tina ikatolewa Julai 12, 2017. Akahukumiwa miaka minne jela,” imeelezwa.

Kuna mkakati wa kumpoteza Killel?
Killel anajulikana kwa msimamo wake wa kuiunga mkono Serikali katika kuhakikisha migogoro ya ardhi Loliondo inamalizwa.
Wakati wa Kamati iliyoundwa kwa maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha migogoro inamalizwa, Killel alitoa mchango mkubwa kwa kuamua kuwa muwazi.
Alieleza mbinu zinazotumiwa na NGOs kujikusanyia mabilioni ya shilingi kutoka ughaibuni, akisema hicho ndicho chanzo kikuu cha kutomalizika kwa migogoro katika eneo hilo.
Kwa muda mrefu amekuwa kwenye mzozo na mmoja wa wafadhili wakuu wa NGos hizo, akiwamo Sussana Nordland. Huyo ni miongoni mwa wanaotajwa kugharimia kesi zinazofunguliwa dhidi ya watu wanaopinga uchochezi unaofanywa na NGOs.

Baada ya Killel kuhukumiwa kifungo, alieleza kufurahishwa kwake na hatua hiyo.
Sussana amekuwa na ukaribu na Tina pamoja na Maanda Ngoitiko, ambao wote wawili asili yao ni Kenya. Mwaka 2015, Tina alitumiwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere kueleza kile alichodai kuwa ni wananchi kunyang’anywa ardhi yao na mwekezaji – Kampuni ya Otterlo Business (OBC); jambo ambalo si la kweli.